Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

JIANG YUNTAO: TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA WADAU WOTE KUFIKIA DIRA 2050

 


Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam

Mwenyekiti wa CRJE (E.A) LTD na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Makampuni ya Kichina Nchini Tanzania (CEAT), Bw. Jiang Yuntao, ameahidi kuwa CRJE itaendelea kushirikiana bega kwa bega na wadau kutoka sekta zote nchini Tanzania kuunga mkono utekelezaji wa DIRA 2050.

Akizungumza katika Jukwaa la Maendeleo ya Kimataifa la Makampuni – Tanzania (Phoenix Global Development Forum for Enterprises–Tanzania), lililofanyika kwa mafanikio Oktoba 3, 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, na kuandaliwa kwa pamoja na Phoenix TV na CEAT kwa kaulimbiu ya "Kugundua Afrika Mpya, Kuchunguza Fursa Mpya," Bw. Jiang alisema makampuni ya Kichina yataendelea kuunga mkono juhudi kubwa za kuleta maendeleo nchini Tanzania.

Jukwaa hilo lilihudhuriwa na wageni takriban 100 kutoka serikalini, sekta binafsi na vyuo vikuu. Miongoni mwa wageni wa heshima waliohudhuria na kutoa hotuba za ufunguzi walikuwa Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji; Bw. Shigeki Komatsubara, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania; na Mhe. Chen Mingjian, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania.

Bw. Jiang alieleza kuwa historia ya CRJE nchini Tanzania inaanzia kwenye Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA), ambapo tangu mwaka 1969 kampuni mama ya CRJE, China Railway Construction Engineering Group (CRCEG), ilituma wafanyakazi 1,114 kushiriki ujenzi wa reli hiyo, ikijenga takriban mita za mraba 506,400 za majengo mbalimbali ikiwemo vituo 93, viwanda vya matengenezo, shule za ufundi, hospitali na miundombinu mingine.

Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 2025 inalenga kujenga Tanzania iliyo na ustawi, haki, ushirikishwaji na kujitegemea ifikapo 2050, ikiungwa mkono na hatua muhimu kama kutiwa saini kwa mradi wa uhuishaji wa TAZARA Septemba 2025 na tamko la pamoja la China, Tanzania na Zambia Novemba 2025 la kujenga Ukanda wa Ustawi wa TAZARA.

Kuhusu namna CRJE itakavyounga mkono DIRA 2050, Bw. Jiang alisema kampuni itaendelea kuimarisha misingi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia miundombinu inayohusisha ujenzi wa nyumba, barabara, viwanja vya ndege, umeme, maji, umwagiliaji, bandari na uwekezaji.

Alitaja miongoni mwa miradi iliyotekelezwa kuwa ni hoteli za nyota tano ikiwemo Kilimanjaro Hotel jijini Dar es Salaam, Gran Melia Arusha na Park Hyatt Zanzibar, pamoja na Daraja la Nyerere linalounganisha Kurasini na Kigamboni, Bandari ya Mtwara, mradi wa umwagiliaji wa Iringa, laini za umeme Geita, jengo la VIP Terminal 1 lililokamilika ndani ya siku 75, Hoteli ya Johari Rotana, majengo ya Victoria Nobel na Peninsula Noble, na Uwanja wa Arusha unaojengwa kwa ajili ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani.

Alisema CRJE imeendelea kutoa kipaumbele kwa ajira za wazawa, ambapo Watanzania wanachukua zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi katika miradi yake, kupitia mafunzo ya uanagenzi na Programu ya Kukuza Vipaji ya Ufundi wa Kichina kwa Vijana wa Tanzania iliyozinduliwa hivi karibuni.

"Nyakati zinabadilika, sekta zetu za biashara zinabadilika, na miradi inabadilika – lakini dhamira yetu ya asili ya kuendelea pamoja na Tanzania haijawahi kubadilika," alisisitiza.

Post a Comment

0 Comments