Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini imeongeza muda wa leseni ya uchimbaji mgodi wa Barrick North Mara uliopo katika wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa kipindi cha miaka 15 kuanzia mwaka huu.Uhuishaji huu wa leseni unamaanisha kuwa North Mara itaendelea kuwekeza katika mgodi huo, wafanyakazi wake,na jamii zinazouzunguka kwa kipindi kirefu zaidi.
Tangu Barrick ilipoanza kuendesha shughuli zake nchini mwaka 2019, Mgodi wa Barrick North Mara umefanikisha kuongeza ajira kwa wazawa, kupanua manufaa ya kiuchumi kwa jamii zinazoishi jirani, na kuimarisha uhusiano wake na wadau wa eneo hilo. Hivi sasa, Watanzania wanaunda asilimia 96 ya nguvukazi ya takriban watu 3,000 , huku asilimia 47 wakitoka katika jamii zinazouzunguka mgodi huo.
Barrick imeingiza takriban dola bilioni 5.3 katika uchumi wa Tanzania tangu mwaka 2019, ikiwemo dola bilioni 1.2 mwaka 2025 pekee kupitia kodi, mirabaha, mishahara, gawio na ununuzi wa bidhaa na huduma nchini. Ushiriki wa wenyeji unasalia kuwa nguzo muhimu, huku zaidi ya asilimia 90 ya manunuzi yakifanywa kutoka kwa kampuni zilizosajiliwa Tanzania, ambazo nyingi ni za wazawa. Mwaka 2025, Barrick ilitunukiwa tuzo kadhaa na Serikali ya Tanzania, ikiwemo tuzo ya mlipaji bora wa gawio na mchangiaji mkubwa zaidi wa mapato ya serikali.
"Hii ni hatua muhimu kwa mgodi wa North Mara na kwa ushirikiano wetu na Tanzania," alisema Seb Bock, Afisa Mtendaji Mkuu wa kitengo cha biashara cha Barrick kinachoshughulikia maeneo mengine ya dunia (Rest of World). "Tangu mwaka 2019, tumeshirikiana na Serikali ya Tanzania pamoja na jamii za maeneo husika kujenga ushirikiano imara zaidi na kuleta fursa zaidi kwa Watanzania wote. Kiini cha biashara yetu ni kujenga ushirikiano wa dhati na wenye kuaminiana na wadau wote, na hatua hii ya kuhuisha ushirikiano inaakisi dhamira hiyo."
Barrick na Serikali ya Tanzania zilianzisha kampuni ya Twiga Minerals mwaka 2019 ili kuendesha kwa pamoja migodi ya North Mara na Bulyanhulu. Serikali inamiliki hisa za asilimia 16 katika kila mgodi, na washirika hao wawili hugawana faida ya kiuchumi kwa usawa. Kamati za Maendeleo ya Jamii husaidia kuamua ni miradi ipi ya eneo husika ipewe kipaumbele, kama vile shule, zahanati na barabara.
"Mahusiano katika mgodi wa North Mara yameimarika tangu Barrick ilipochukua uendeshaji," alisema Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele. "Sasa wakazi wanauona mgodi huo kama mshirika wa jamii."

0 Comments