Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

MRADI WA MAJI BILIONI 82.8 SHINYANGA WAANZA, SHUWASA YAMPA CCECC KIBALI CHA KUANZA KAZI RASMI

  

Washiriki wa kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kikao. Picha na Kadama Malunde
Kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga kikiendelea, kikihusisha SHUWASA, mkandarasi CCECC na kampuni ya usimamizi wa mradi. Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Usimamizi wa Mradi, Artelia S.A.S, Klaus Buchholtz, akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga wenye thamani ya Shilingi bilioni 82.8.
Mwanasheria wa SHUWASA, Happy Richard, akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga.
Meneja wa Mradi wa Maji wa CCECC, Adam Zhou (katikati), akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imetoa kibali rasmi kwa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kuanza utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 82.8, unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na kuimarisha miundombinu ya maji katika maeneo mbalimbali ya Shinyanga.

Hatua hiyo imefikiwa kupitia kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa mradi, ambapo SHUWASA na wadau wa mradi wamejadili na kuweka makubaliano ya utekelezaji wa kazi kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa Machi 24, 2026 kati ya SHUWASA na CCECC.

Akizungumza katika kikao hicho leo Oktoba 6,2026, Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, amesema mradi huo ni sehemu ya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji unaolenga kuongeza uwezo wa utoaji wa huduma, kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji pamoja na kupunguza upotevu wa maji unaotokana na uchakavu wa miundombinu.

Mhandisi Katopola amesema mkataba huo wenye thamani ya Euro milioni 29.28, sawa na Shilingi bilioni 82.87, unahusisha ujenzi wa mtandao mpya wa maji safi wenye urefu wa takribani kilomita 278, ukarabati wa mtandao chakavu wenye urefu wa takribani kilomita 100, pamoja na ujenzi wa matenki mawili makubwa ya kuhifadhia maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola.

Kwa mujibu wa SHUWASA, tanki moja litajengwa katika eneo la Kolandoto likiwa na uwezo wa kuhifadhi lita 1,500,000, wakati tanki jingine litajengwa katika eneo la Didia likiwa na uwezo wa kuhifadhi lita 250,000.

“Leo hii tumefanya kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira. Leo tumefanya kikao kizuri sana cha kumruhusu mkandarasi aanze kazi rasmi ya ujenzi. Tayari mkandarasi yupo site na ameshaanza kazi,” amesema Mhandisi Katopola.

Mkurugenzi huyo ametumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za Serikali katika kuhakikisha rasilimali fedha zinapatikana kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini, ikiwemo mradi huo wa Shinyanga.

Kwa mujibu wa Katopola, fedha za mradi huo zinatokana na ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kupitia mkopo wenye masharti nafuu, unaosaidia kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira.

“Tunatumia nafasi hii kumshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kututafutia fedha, kwa sababu fedha hizi ni fedha za mkopo wa riba nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa ambalo pamoja na Serikali ya Muungano wa Tanzania zimetupatia fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu wa maji,” amesema Katopola.

Amesema uwekezaji huo utakuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi kutokana na maboresho yatakayofanyika katika miundombinu ya maji, hususan mabomba chakavu ambayo yamekuwa chanzo cha upotevu wa maji na wakati mwingine kusababisha wananchi kukosa huduma katika vipindi mbalimbali.

“Miongoni mwa kazi zitakazofanywa na mkandarasi ni kufanya ukarabati mkubwa wa mtandao wa maji ambao sisi SHUWASA tunautumia, ambapo tunaenda kutoa mabomba ambayo yamekuwa yakipelekea wananchi wa eneo la Manispaa ya Shinyanga kukosa maji katika baadhi ya vipindi na kusababisha upotevu wa maji,” amesema.
Katopola amesema SHUWASA tayari inaendelea na juhudi za kudhibiti upotevu wa maji, lakini mradi huo utatoa fursa ya kuimarisha zaidi hatua hizo na kuongeza ufanisi wa huduma.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Katopola amemshukuru Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, kwa kuendelea kusimamia na kuunga mkono utekelezaji wa miradi ya maji nchini, akisema mradi wa Shinyanga ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi.

“Lakini pia nitumie fursa hii kumshukuru Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, kwa kuendelea kusimamia na kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya maji nchini. Kwa kweli tunaendelea na utekelezaji wa mradi huu, ambao tunatarajia utakapokamilika utaboresha kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa huduma ya maji safi kwa wananchi wa Shinyanga, kuongeza uwezo wa SHUWASA wa kutoa huduma na kupunguza changamoto zinazotokana na uchakavu wa miundombinu ya maji,” amesema Mhandisi Katopola.

CCECC YAAHIDI KUKAMILISHA MRADI KWA MIEZI 36

Kwa upande wake, Mhandisi Mkuu wa CCECC, Newton Wilson Semiti, akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Mradi, Adam Zhou, amesema kampuni hiyo imejipanga kukamilisha utekelezaji wa mradi huo ndani ya kipindi cha miaka mitatu kama ilivyoainishwa kwenye mkataba.
Mhandisi Mkuu wa CCECC, Newton Wilson Semiti.

Amesema CCECC ina uwezo wa rasilimali watu, vifaa na fedha unaohitajika kuhakikisha kazi inakamilika ndani ya muda uliopangwa.

“Mradi huu utachukua miaka mitatu katika utekelezaji. Kama kampuni tunaahidi ndani ya miaka mitatu tutakuwa tumemaliza mradi kwa sababu nguvu tunazo na fedha za mradi zipo,” amesema Semiti.

Aidha, amesema mradi huo unatarajiwa kutoa ajira kwa wananchi wa Shinyanga, ambapo hadi sasa kampuni hiyo imeajiri mainjinia wazawa 16 pamoja na wafanyakazi 145 wasio na utaalamu (unskilled labour) wanaofanya kazi katika eneo la mradi.

Amesema idadi hiyo itaongezeka kadiri utekelezaji wa mradi utakavyoendelea, huku CCECC ikilenga kuajiri takribani wafanyakazi 250, hasa kutoka Shinyanga, ili wananchi wa eneo hilo wanufaike moja kwa moja na fursa zinazotokana na mradi.

WASIMAMIZI WA MRADI WAWEKA MKAZO KWENYE UBORA

Naye Mhandisi Mkazi (Resident Engineer)wa kampuni ya usimamizi wa mradi, Artelia S.A.S, Klaus Buchholtz, amesema kampuni hiyo imepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi kwa ishirikiana na Kampuni ya LUPTAN Consult & ENGTECH Tanzania Ltd kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.

Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Usimamizi wa Mradi, Artelia S.A.S Klaus Buchholtz

Amesema usimamizi huo utazingatia masuala ya kiufundi, mazingira, afya na usalama, ili kuhakikisha kazi zinazotekelezwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Mradi huo unasimamiwa na ARTELIA S.A.S kwa kushirikiana na LUPTAN Consult & ENGTECH Tanzania Ltd, huku SHUWASA ikiwa ndiye mteja na CCECC akiwa mkandarasi.

Mkataba huo uliosainiwa Machi 24, 2026 unatarajiwa kukamilika Machi 23, 2029, sawa na kipindi cha siku 1,095 au miezi 36.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza na kuboresha miundombinu ya maji safi kupitia ujenzi wa mtandao mpya wa kilomita 278, ukarabati wa takribani kilomita 100 za mtandao chakavu pamoja na ujenzi wa matenki mawili ya kuhifadhia maji katika maeneo ya Kolandoto na Didia.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga wenye thamani ya Shilingi bilioni 82.8.
Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Usimamizi wa Mradi, Artelia S.A.S, Klaus Buchholtz, akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga.
Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Usimamizi wa Mradi, Artelia S.A.S, Klaus Buchholtz, akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga.
Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Usimamizi wa Mradi, Artelia S.A.S, Klaus Buchholtz, akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga.
Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Usimamizi wa Mradi, Artelia S.A.S, Klaus Buchholtz, akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga.

Post a Comment

0 Comments