NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, ametoa wito wa kuimarishwa kwa huduma za tiba shufaa nchini ili kupunguza mateso ya wagonjwa wenye magonjwa yanayotishia maisha na kuhakikisha wanapata huduma kwa heshima na wakati unaofaa.
Pinda amesema tiba shufaa haipaswi kuonekana kama huduma ya mwisho baada ya matibabu mengine kushindikana, bali inapaswa kuanza mapema na kutolewa sambamba na matibabu mengine pale inapohitajika.
Amesema mfumo bora wa afya haupaswi kupimwa kwa uwezo wa kutibu na kuponya pekee, bali pia kwa uwezo wa kupunguza maumivu na mateso ya wagonjwa pamoja na kulinda utu wao.
“Tunapozungumzia tiba shufaa, tunazungumzia zaidi ya matibabu ya ugonjwa. Tunazungumzia namna ya kumsaidia mtu anayeishi na ugonjwa unaotishia maisha au unaomsababishia mateso makubwa kuendelea kuishi kwa heshima, kupunguza maumivu na dalili nyingine,” amesema.
Pinda ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika Kongamano la Nne la Kisayansi la Huduma ya Tiba Shufaa na Afya ya Jamii Afrika Mashariki (EAPCON 2026).
Amesema ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo saratani, magonjwa ya moyo, kisukari na magonjwa ya figo, linaongeza umuhimu wa kuimarisha huduma za tiba shufaa katika jamii.
Amesema Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa ni takribani asilimia 14 pekee ya watu wanaohitaji tiba shufaa duniani wanaopata huduma hiyo, hali inayodhihirisha ukubwa wa pengo lililopo.
Amesema Tanzania inapaswa kuendelea kuimarisha huduma hiyo katika ngazi mbalimbali za afya, kujenga uwezo wa watoa huduma na kuongeza upatikanaji wa huduma za kudhibiti maumivu, ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia.
Pinda ametaja maeneo matano yanayohitaji kupewa kipaumbele, likiwemo kuhakikisha tiba shufaa inakuwa sehemu ya mfumo wa huduma za afya katika vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa.
Amesema pia kuna umuhimu wa kuimarisha udhibiti wa maumivu na dalili nyingine zinazowasababishia wagonjwa mateso, huku akisisitiza kuwa wagonjwa wenye uhitaji halali wanapaswa kupata dawa muhimu kwa wakati.
Eneo jingine ni kuwekeza katika rasilimali watu, ambapo amesema madaktari, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa afya ya jamii, wanasaikolojia na wataalamu wa ustawi wa jamii wanahitaji kuwa na ujuzi wa kutambua na kushughulikia mahitaji ya wagonjwa wanaohitaji tiba shufaa.
Aidha, amesisitiza matumizi ya ushahidi wa kisayansi katika kupanga na kuboresha huduma, akisema tafiti zinapaswa kusaidia kuelewa ukubwa wa mahitaji, changamoto za upatikanaji wa huduma na dawa pamoja na mahitaji ya wagonjwa, familia na watoa huduma.
Pinda pia ameitaka jamii kutambua nafasi ya familia na walezi katika tiba shufaa, kwa kuwa wagonjwa hutumia muda mwingi wakiwa nyumbani na familia ndiyo inayobeba sehemu kubwa ya jukumu la kuwahudumia.
Kwa upande wa Afrika Mashariki, amesema nchi wanachama zinapaswa kutumia EAPCON kama jukwaa la kubadilishana uzoefu, kufanya tafiti za pamoja, kujenga uwezo wa wataalamu na kutafuta suluhisho la changamoto zinazofanana katika utoaji wa huduma.
“Nyuma ya kila takwimu kuna mtu mwenye jina, familia na historia yake. Tiba shufaa inalenga kuhakikisha kuwa mtu hasahauliki kwa sababu ugonjwa wake ni mkubwa, wa muda mrefu au hauwezi kuponywa,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea, amesema huduma za tiba shufaa licha ya kuwepo kwa muda mrefu nchini, bado hazijapewa uzito unaostahili katika maeneo mbalimbali ya utoaji wa huduma za afya.
Amesema hali hiyo inafanya mzigo mkubwa wa kuwahudumia wagonjwa kubaki kwa wagonjwa wenyewe na familia zao.
Nyembea amesema madaktari na wataalamu wa afya hawawezi kuzuia kifo katika kila hali, lakini wana uwezo wa kupunguza maumivu, kuboresha maisha ya wagonjwa wenye magonjwa sugu na kuwasaidia wagonjwa kufikia mwisho wa maisha yao kwa heshima.
Amesema Tanzania hugundua takribani wagonjwa wapya 42,000 wa saratani kila mwaka, huku takribani 29,000 wakifariki kutokana na ugonjwa huo kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Nyembea, zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wanaogundulika kuwa na saratani nchini hufika katika vituo vya huduma wakiwa katika hatua za juu za ugonjwa, hasa hatua ya tatu na ya nne.
Amesema hali hiyo inaongeza umuhimu wa kuimarisha tiba shufaa ili wagonjwa wanaofika katika hatua hizo waweze kupata huduma zinazolenga kupunguza maumivu, kuboresha maisha na kuwasaidia wao pamoja na familia zao kukabiliana na hali ya ugonjwa.
Amesema kuimarisha huduma hiyo kunahitaji ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu wa afya, taasisi za mafunzo, watafiti, mashirika ya kitaaluma, familia na jamii kwa ujumla.
0 Comments