Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

SERIKALI YAIMARISHA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI KATIKA VITALU MBALIMBALI NCHINI

Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara, umekamilika kwa mafanikio na kugundua gesi inayotarajiwa kuongeza akiba ya taifa inayokadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 57.54.

Amesema Serikali inatarajia kuzindua visima hivyo wiki ijayo katika Kijiji cha Msimbati, mkoani Mtwara, ambapo pia itatangaza rasmi kiasi cha gesi kilichogunduliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 18, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Homera amesema visima hivyo, viwili vya uendelezaji na kimoja cha utafiti, vimechimbwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na kampuni ya M&P.

Amesema ugunduzi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa nchi kukidhi mahitaji ya nishati na kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi asilia.

Homera amesema Serikali kupitia TPDC inaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Eyasi-Wembere, Lindi-Mtwara, Songo Songo Magharibi, Mnazi Bay Kaskazini na Ntorya.

Ameeleza kuwa uchukuaji wa data za mitetemo unaendelea katika vitalu vya Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu, huku maandalizi ya uchimbaji wa kisima cha uzalishaji na usimikaji wa mitambo ya kusafisha gesi yakiendelea katika Kitalu cha Ntorya.

Kuhusu Ntorya, amesema ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi lenye urefu wa kilomita 35 kutoka eneo hilo hadi Madimba umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026.

Amesema uzalishaji wa gesi katika eneo hilo unatarajiwa kuanza mapema mwaka 2027, ukiwa na uwezo wa kufikia futi za ujazo milioni 40 kwa siku.

Katika hatua nyingine, Homera amesema TPDC inaendelea kushirikiana na kampuni binafsi kusambaza gesi asilia majumbani na kwenye magari kupitia mfumo wa gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG). Hadi Septemba 2026, jumla ya vituo 22 vilikuwa vimekamilika na kuanza kutoa huduma.

Aidha, amesema Serikali inatarajia kusaini na kukabidhi leseni mpya za mikataba ya uzalishaji kwa kugawana mapato (PSA) kwa TPDC wiki ijayo, hatua itakayoliwezesha shirika hilo kuendeleza shughuli za utafutaji, uzalishaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi nchini. Hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, kama mgeni rasmi.

Akizungumzia sekta ya umeme, Homera amesema uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini umefikia megawati 4,646 kutoka vyanzo mbalimbali, vikiwemo maji, gesi asilia, jua na nishati nyingine mbadala.

Amesema Serikali inalenga kuongeza uwezo huo hadi megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukidhi mahitaji ya umeme yanayoongezeka nchini.

Ameongeza kuwa Serikali imekamilisha Mradi wa Kishapu I wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50 za umeme wa jua, huku ujenzi wa Kishapu II wenye uwezo wa megawati 100 ukiendelea. Miradi mingine ya umeme wa jua yenye uwezo wa zaidi ya megawati 600 ipo katika hatua mbalimbali za majadiliano na upembuzi.

Kuhusu usafirishaji wa umeme, amesema Mradi wa Chalinze–Dodoma umekamilika tangu Septemba 2026 na umeimarisha ubora na kiwango cha umeme kinachofika katika mikoa ya Magharibi na Kaskazini mwa nchi.

Amesema Mradi wa Iringa–Tunduma–Sumbawanga unatarajiwa kuwashwa Novemba mwaka huu, hatua itakayoiunganisha Rukwa katika Gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza.

Vilevile, Mradi wa Chalinze–Kinyerezi–Mkuranga unatarajiwa kuwashwa Februari 2027 kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam na katika maeneo ya viwanda ya Mkuranga.

Amesema utekelezaji wa Mradi wa Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika unaendelea kwa kasi, ukiwa na lengo la kuunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa na kuboresha upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo.

Post a Comment

0 Comments