WATAALAMU wa manunuzi na ugavi wametakiwa kuzingatia maadili, sheria na taratibu za taaluma hiyo ili kudhibiti upotevu wa fedha za umma na kuhakikisha Serikali inapata thamani halisi ya fedha katika ununuzi wa bidhaa na huduma.
Akizungumza katika mahafali ya 15 ya wataalamu wa manunuzi na ugavi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Deogratius Luswetula, amesema wataalamu hao wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji, huku wakiepuka vitendo vya udanganyifu na mgongano wa maslahi.
Amesisitiza kuwa uzingatiaji wa maadili ya taaluma hiyo ni muhimu katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (PSPTB), Jacob Kibona, amesema bodi hiyo inaendelea kuboresha mitaala, kutoa mafunzo endelevu na kuimarisha usimamizi wa taaluma ili kuongeza ufanisi katika sekta ya manunuzi na ugavi.
Naye Kaimu Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma Serikalini, Alex Haraba, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na bodi, vyuo na waajiri kuongeza idadi ya wataalamu wenye sifa na kuhakikisha nafasi za manunuzi zinajazwa na watumishi waliokidhi vigezo vya kitaaluma.
Kwa upande wake, mhitimu wa programu hizo, Ismael Kagungu, amesema wahitimu watatumia maarifa na ujuzi walioupata kuimarisha uwazi, ushindani na matumizi bora ya fedha za umma.
0 Comments