BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imewawezesha wateja wake 14 kwenda nchini Japan kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya J-AGRI Tokyo, kwa lengo la kujifunza teknolojia na ubunifu unaoweza kuongeza tija katika sekta ya kilimo nchini.
Ziara hiyo inafanyika ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 yenye kaulimbiu “The Extra Mile”, inayosisitiza umuhimu wa kwenda hatua ya ziada katika kuwahudumia wateja.
Kupitia maonesho hayo, wateja hao wanapata fursa ya kujifunza na kuona kwa vitendo teknolojia mbalimbali zinazotumika katika kilimo, ikiwamo mashine za kilimo, mifumo ya umwagiliaji, kilimo janja, matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones), pamoja na teknolojia za kuhifadhi na kusafirisha mazao.
Aidha, washiriki hao wanakutana na wazalishaji na wasambazaji wa vifaa na teknolojia za kilimo kutoka Japan, hatua inayolenga kuwasaidia kutafuta teknolojia zinazoweza kuendana na mahitaji ya wakulima na wafanyabiashara wa kilimo nchini Tanzania.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, alisema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa benki kwenda zaidi ya utoaji wa mikopo kwa kuwawezesha wateja kupata maarifa, teknolojia na uzoefu wa kimataifa.
Alisema TADB inaamini kuwa kuwawezesha wateja kupata fursa za kujifunza kutoka katika nchi zilizoendelea kiteknolojia kutawasaidia kuongeza tija, kuboresha ubora wa bidhaa na kuongeza thamani katika shughuli zao za kilimo.
“The Extra Mile inatukumbusha umuhimu wa kwenda hatua ya ziada katika kuwahudumia wateja wetu. Hatutaki kuwawezesha kifedha pekee, bali pia kuwapatia maarifa na fursa zinazoweza kuwasaidia kukuza biashara zao,” alisema Nyabundege.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wateja hao, Kamal Simba, aliishukuru TADB kwa kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo, akisema wanatarajia kurejea nchini wakiwa na maarifa na uzoefu utakaosaidia kuboresha shughuli zao.
Wateja hao 14 wanajihusisha na shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa kilimo, zikiwamo usindikaji wa mazao, uendeshaji wa maghala, ununuzi wa mazao, mitambo, pembejeo na huduma za umwagiliaji.
Kwa pamoja, wamewezeshwa na TADB mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 62, huku fursa hiyo ya kwenda Japan ikilenga kuwaongezea uelewa wa teknolojia na ubunifu utakaowasaidia kuongeza tija, ufanisi na thamani katika shughuli zao.
TADB imeeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwezo wa wateja wake na kuchochea matumizi ya teknolojia katika mnyororo wa thamani wa kilimo, kwa lengo la kuongeza uzalishaji na ushindani wa bidhaa za Tanzania.
0 Comments