Afisa Msimamizi wa Afya, Usalama, Ulinzi na Mazingira wa Kampuni ya Taifa Gas, Aurelius Mdemu (kulia), akikabidhi mtungi wa gesi kwa mmoja wa washiriki wa semina ya matumizi salama ya nishati safi ya kupikia iliyowalenga wanawake na wanaume wenye ulemavu na mahitaji maalum jijini Dar es Salaam.
Afisa Masoko wa Kampuni ya Taifa Gas, Santina Ngaponda (katikati), akipokea cheti cha udhamini wa semina ya matumizi ya nishati safi kwa watu wenye ulemavu jijini Dar es Salaam. Pembeni yake ni Mwakilishi wa Kampuni ya Badson Group, Francis Ngonga, na Mkurugenzi wa Tupo Sawa Organization, Jackline Mtaita, aliyeketi kwenye kiti cha magurudumu. Semina hiyo iliandaliwa na Tupo Sawa Organization na kudhaminiwa na Taifa Gas.
Msimamizi wa Afya, Usalama na Mazingira wa Kampuni ya Taifa Gas, Aurelius Mdemu, akimkabidhi mtungi wa gesi Happiness Alberto wakati wa semina ya siku moja kuhusu matumizi salama ya nishati safi ya kupikia kwa watu wenye ulemavu na mahitaji maalum, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa semina ya matumizi salama ya nishati safi ya kupikia kwa watu wenye ulemavu na mahitaji maalum wakifuatilia mafunzo yaliyotolewa na wataalamu jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa semina ya matumizi salama ya nishati safi ya kupikia kwa watu wenye ulemavu na mahitaji maalum wakifuatilia mafunzo yaliyotolewa na wataalamu jijini Dar es Salaam.
**
Kampuni ya Taifa Gas imedhamini na kushiriki kutoa mafunzo ya siku moja kuhusu matumizi ya nishati safi kwa watu wenye ulemavu na mahitaji maalum yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Tupo Sawa Organization na kufanyika jijini Dar es salaam yakiwa na kauli mbiu ya Jasiri Energy.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na walemavu na walezi wa watoto wenye ulemmavu zaidi ya 100 ambapo walipata fursa ya kupata elimu ya matumizi ya nishati safi kutoka kwa wataalamu ambapo pia waligawiwa mitungi ya gesi kutoka kampuni ya Taifa Gas.
Afisa Msimamizi wa Afya , Usalama , Ulinzi na Mazingira wa Taifa Gas , Aurelius Mdemu amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya nishati salama na kuwawezesha kutambua ujazaji haramu wa gesi (Illegal Refill) unaowafnywa na watu wasio waaminifu ili kuwaepusha na majanga ya moto kwenye maeneo yao ya biashara na majumbani.
Mdemu alieleza kuwa pamoja na mambo mengine semina hiyo ilikuwa ni muendelezo wa kuwahamasisha watanzania kuacha matumizi ya mkaa na ukataji wa kuni katika jitihada za kuendelea kulinda mazingira na uoto wa asili kwa maslahi mapana ya taifa.
Enock Ngulwa , Meneja Mauzo wa Mkoa wa Dar es Salaam wa Taifa Gas alisema kwamba watu wenye mahitaji maalum ni muhimu kwenye jamii kupata uelewa wa matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia na kuongeza uelewa wa jinsi mitungi ya gesi inavyouzwa kwenye masoko hapa nchini.
“Ni muhimu kwa makundi maalum kwenye jamii ya watanzania kupata uelewa wa matumizi sahihi ya mitungi ya gesi , usalama , afya na kulinda mazingira pamoja na uuzwaji wa gesi unavyofanyika kwenye masoko yanayotambulika kwa mujibu wa sheria,” alisema Ngulwa.
Aliongeza kwamba semina hiyo lengo lingine ni kuwafundisha jinsi ya kutumia gesi kwa usahihi na kulinda usalama kwenye maeneo wanapoishi pamoja na kuwa mabalozi wazuri kwenye kueneza elimu ya matumizi ya nishati ya safi katika juhudi za kulinda mazingira.
Ngulwa alisema wameamua kuwashirikisha kada hiyo kwa sababu ni sehemu ya jamii na ni muhimu kuwapa semina ya kujilinda na madhara yanayoweza kuepukika katika matumizi ya mitungi ya gesi.
Kwa upande wake , Mkurugenzi wa Tupo Sawa Organization , Jackline Mtaita, alisema kuwa shirika hilo litaendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali kwenye kuhamasisha watanzania kutumia nishati safi kwa ajili ya kupikia ili kuendelea kulinda mazingira nchini.
“Nachukua nafasi hii kutoa shukrani kwa kampuni ya Taifa Gas kwa kudhamini semina hii muhimu kwa watu wenye ulemavu katika harakati za kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais , Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye matumizi ya nishati safi,” alisema Bi Mtaita.
Alisema kwamba watu wenye ulemavu wana na haki ya kuwezeshwa kupata elimu jumuishi ikiwa na pamoja ya matumizi ya nishati safi na kujihusisha na biashara za uuzaji wa mitungi ya gesi katika kukabiliana na changamoto za kipato.
Mjasiriamali na mlemavu, Happiness Alberto ambaye anajishughulisha na utengenezaji wa keki kwenye eneo la Mbezi Goba alisema kwamba semina hiyo ni fursa muhimu kwao kwa ajili ya kujifunza matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia katika kulinda mazingira,afya zao na kuokoa muda.
Kampuni ya Taifa Gas ilitumia fursa hiyo pia kugawa mitungi ya gesi kwa watu wenye ulemavu na uhitaji kwa ajili ya kuongeza kasi ya kampeni ya matumizi ya nishati safi nchini.
Serikali ya awamu ya sita na wadau mbalimbali nchini huendesha programu za utoaji wa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia mahususi kwa makundi maalumu ikiwemo watu wenye ulemavu ili kuhakikisha hawabaki nyuma katika mageuzi ya nishati.
Malengo ya Elimu ya Nishati Safi kwa Watu Wenye Ulemavu
Kulinda Afya: Kuokoa watumiaji dhidi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji na madhara yatokanayo na moshi wa kuni na mkaa.
Usalama Jikoni: Kutoa mafunzo ya matumizi ya teknolojia rafiki na majiko banifu yaliyo salama zaidi kwa watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali (kama vile viziwi au watu wenye ulemavu wa viungo).
Kujumuishwa Kiuchumi: Kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki shughuli za ujasiriamali kupitia vikundi na kusambaza au kutumia nishati nafuu.
Wizara ya Nishati: Inaratibu Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) unaolenga kufikia asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034.






0 Comments