Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

Tanzania yazindua Zoezi la Utoaji Elimu kwa Umma Kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la EAC

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi zoezi la utoaji elimu kwa umma kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha uelewa na ushiriki wa Wananchi katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa ushirikiano wa kikanda.

Uzinduzi huo umefanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Ngeleja Kadonya, jijini Dodoma, Oktoba 26, 2026. Zoezi hilo linatarajiwa kutekelezwa kuanzia Oktoba 26 hadi Novemba 2, 2026, likihusisha maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Dodoma, Mwanza, Arusha, Kigoma, Mbeya, Dar es Salaam, Mtwara na Zanzibar.

Zoezi hilo linalenga kuwawezesha wananchi kuelewa kwa kina maudhui ya rasimu hiyo, umuhimu na mchangao wake kwa maendeleo ya Tanzania na wananchi wa Afrika Mashariki, ili washiriki kikamilifu kwa kutoa maoni yenye tija yatakayozingatia maslahi ya Taifa na Jumuiya kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu Bw. Kadonya amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika zoezi hilo, akieleza kuwa Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa inahusu masuala ya msingi yanayogusa maisha ya kila siku ya wananchi na mustakabali wa ushirikiano wa kikanda.

Amebainisha kuwa miongoni mwa masuala yanayohitaji uelewa na mchango wa wananchi ni pamoja na; masuala ya utawala na mgawanyo wa mamlaka baina ya Serikali za Nchi Wanachama, haki za wananchi na ulinzi wao; Ushirikiano wa kiuchumi, pamoja na masuala ya Ulinzi na Usalama.

Aidha, ameeleza kuwa kuwa nchini Tanzania, mchakato huo utatekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza inahusu kutoa elimu kwa umma kuhusu rasimu ya katiba, maudhui yake na umuhimu wake. 

Awamu ya pili itahusisha ukusanyaji wa maoni ya wananchi, ambapo timu ya wataalamu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaohusika na uandaaji wa rasimu hiyo itakutana na wadau katika maeneo yatakayopangwa kwa ajili ya zoezi hilo.

Fungamano la Kisiasa inatazamwa kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala ya utawala, uchumi, usalama na maendeleo ya kikanda.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi na watendaji mbalimbali wa Serikali, wakiwemo Makatibu Wakuu, Waheshimiwa Majaji, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma, Wakuu wa Taasisi za Serikali na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo.

Post a Comment

0 Comments