Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

NDEJEMBI AHIMIZA NISHATI SAFI, LAKE GAS NA MAMA SALMA WAGAWA MITUNGI YA KUPIKIA

 


Na Mwandishi Wetu, Mchinga

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yana faida kwa afya, mazingira na uchumi wa kaya, akieleza kuwa matumizi ya gesi yanapunguza athari za moshi unaotokana na kuni na mkaa pamoja na gharama za upishi.

Amesema hayo wakati wa zoezi la ugawaji wa sehemu ya mitungi 750 ya gesi yenye ujazo wa kilo sita kwa wananchi wa Jimbo la Mchinga, mkoani Lindi, iliyotolewa kwa ushirikiano kati ya Lake Gas chini ya Lake Group na Mbunge wa jimbo hilo, Salma Kikwete.
Ndejembi amesema matumizi ya gesi badala ya kuni na mkaa yatasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira, huku yakilinda afya za wananchi dhidi ya madhara ya kuvuta moshi wakati wa kupika.

“Mitungi hii ya gesi na nishati safi ya kupikia inaenda kulinda afya zetu. Badala ya kupika kwa kutumia mkaa na kuvuta moshi wote unaotokana na upishi, sasa tunaenda kutumia nishati safi ambayo haitadhuru afya zetu,” amesema.

Ameongeza kuwa matumizi ya gesi yanaweza kusaidia kaya kuokoa fedha kutokana na gharama zake kuwa nafuu ikilinganishwa na matumizi ya mkaa.

Amesema ugawaji wa mitungi hiyo ni hatua muhimu katika kuhamasisha wananchi kuachana na nishati zinazochafua mazingira na kuanza kutumia njia salama za kupikia.

Awali, Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete, amesema ushirikiano kati yake na Lake Gas umewezesha upatikanaji wa mitungi hiyo kwa wananchi, ambapo pande hizo zimechangia katika kufanikisha zoezi hilo.

Amesema kampuni hiyo imeunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, sambamba na hatua zilizochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza ajenda hiyo nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mauzo na Masoko wa Lake Gas Tanzania, Sadiq Sabri, amesema kampuni hiyo imeshirikiana na Mbunge wa Mchinga kugawa mitungi 750 yenye ujazo wa kilo sita kwa wananchi wa jimbo hilo.

Amesema mchango huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupanua matumizi ya nishati safi ya kupikia na kufanikisha lengo la kufikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

“Lake Group, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Ally Edha Awadh, tunaunga mkono juhudi za Serikali katika kupanua matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuunga mkono malengo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kufikisha asilimia 80 ya watumiaji wa nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” amesema Sabri.

Zoezi hilo linaongeza juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi, hususan katika kaya ambazo bado zinategemea kuni na mkaa.

Post a Comment

0 Comments