Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

OTR na Newrest zatupia jicho masoko mapya



Na Mwandishi wa OTR - Dar es Salaam.


Kampuni ya kimataifa ya Ufaransa ya huduma za chakula na usimamizi wa huduma mbalimbali, Newrest, imeonesha nia ya kununua hisa zote asilimia 51 zinazomilikiwa na kampuni ya uwekezaji ya Ujerumani, Aurelius, katika Kampuni ya Huduma za Chakula na Vinywaji Ndani ya Ndege (ICSL) yenye makao yake makuu nchini Tanzania.

Hatua hiyo inatarajiwa kupanua shughuli za ICSL nje ya huduma za chakula ndani ya ndege, kampuni ambayo wanahisa wake wengine ni Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) yenye asilimia 40.3 na Taninvest yenye asilimia 8.7.

Nia hiyo ya Newrest ilijadiliwa Jumanne wiki iliyopita katika kikao kati ya Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, na ujumbe wa kampuni hiyo ulioongozwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wake, Bw. Olivier Sadran, katika ofisi za OTR jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilijadili namna uzoefu na utaalamu wa Newrest katika masoko ya kimataifa unavyoweza kukuza ICSL, kupanua vyanzo vyake vya mapato na kuongeza thamani ya uwekezaji wa Serikali katika kampuni hiyo.

Bw. Mchechu alisisitiza kwamba ushirikiano huo unapaswa kuimarisha shughuli zilizopo za ICSL na kutumia fursa mpya katika sekta ambazo Newrest ina uzoefu nazo kimataifa.

"Lengo letu ni kuendeleza biashara iliyopo na kutumia fursa mpya zinazoweza kuimarisha utendaji na thamani ya ICSL kwa muda mrefu," alisema.

Aliongeza kuwa huduma za reli na migodi zinaweza kuwa maeneo muhimu ya kupanua shughuli za kampuni hiyo, kuongeza mapato na kutoa nafasi zaidi kwa kampuni na wataalamu wa Kitanzania kushiriki katika biashara hizo.

Katika sekta ya reli, fursa zilizobainishwa ni pamoja na kutoa huduma za chakula na vinywaji kwa abiria wa Reli ya Kisasa (SGR). Newrest ina uzoefu katika eneo hilo, ikiwemo huduma inazotoa kwa reli ya mwendo kasi ya Al Boraq nchini Morocco.

Sekta ya madini nayo ilitajwa kuwa na fursa, kutokana na mahitaji ya huduma za chakula na huduma saidizi katika migodi iliyo mbali na makazi ya watu.

Kampuni za Barrick na AngloGold Ashanti zilitajwa miongoni mwa waendeshaji wakubwa wa migodi ambao shughuli zao zinaweza kutoa fursa kwa huduma hizo.

Majadiliano hayo pia yalisisitiza umuhimu wa kuzingatia matakwa ya ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi, kwa kujenga ushirikiano utakaowezesha kampuni za ndani kushiriki zaidi katika mnyororo wa ugavi.

Newrest pia iliwasilisha uzoefu ilio nao nchini Angola, ambako inashirikiana na wawekezaji wa ndani wanaobaki kuwa wamiliki wa hisa huku wakinufaika na chapa, utaalamu wa uendeshaji na mifumo ya usimamizi ya kampuni hiyo.

Mfano huo unaonesha namna uwezo wa kampuni za kimataifa unavyoweza kuunganishwa na uwekezaji wa wazawa.

Katika sekta ya usafiri wa anga, mazungumzo yalihusu uwezekano wa kuimarisha ushirikiano na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na kupanua huduma katika maeneo mengine ya kibiashara ndani ya viwanja vya ndege, ikiwemo huduma za chakula na vinywaji na usimamizi wa vyumba maalumu vya mapumziko ya abiria (lounges).

Akieleza ukubwa wa shughuli za Newrest kimataifa, Bw. Sadran alisema kampuni hiyo inafanya kazi katika nchi 51, ina wafanyakazi takribani 65,653, na ilipata mapato ya euro bilioni 3.728 katika mwaka wa fedha 2025/26, ikilinganishwa na euro milioni 196 mwaka 2004/05.

Alisema shughuli za kampuni hiyo zinahusisha huduma za chakula na vinywaji ndani ya ndege, huduma hizo katika maeneo ya mbali, usimamizi wa huduma mbalimbali, huduma za reli na biashara za rejareja.

Akieleza falsafa ya ukuaji wa kampuni hiyo, Bw. Sadran alisema kuvuka mipaka ya kawaida ya utendaji na kutafuta ubora ndio msingi wa namna Newrest inavyoendesha shughuli zake.

Utaalamu wa kampuni hiyo unajumuisha pia mifumo ya teknolojia na uendeshaji, ukiwemo mfumo wa Winrest unaounganisha oda za chakula, manunuzi, usimamizi wa malighafi, mipango ya uzalishaji na usalama wa chakula.

Kwa mujibu wa mwanzilishi wa ICSL, Bw. Paul Lyimo, hatua ya kwanza ya mchakato wa ununuzi tayari imekamilika baada ya Newrest na Aurelius kusaini Hati ya Makubaliano (MoU).


Alisema hatua iliyofuata ilikuwa Newrest kufanya mazungumzo na wanahisa wengine wa ICSL, yaani OTR na Taninvest, ambayo tayari yamefanyika, na sasa kinachosubiriwa ni kusainiwa kwa mkataba rasmi wa ununuzi wa hisa, unaotarajiwa kusainiwa wakati wowote kuanzia sasa.

Bw. Lyimo, anayemiliki hisa hizo asilimia 8.7 kupitia Taninvest, ameikaribisha Newrest, akisema utaalamu wake utaiwezesha ICSL kupanua shughuli zake kutoka huduma za chakula ndani ya ndege hadi sekta nyingine, zikiwemo huduma za chakula kwenye usafiri wa reli na kwenye migodi iliyo maeneo ya mbali.



Post a Comment

0 Comments