
Na Robertha Makinda, WMA – Dodoma
Wakala wa Vipimo (WMA) inashiriki katika Kongamano la Maendeleo Endelevu ya Viwanda lililofunguliwa rasmi tarehe 2 Novemba 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Kongamano hilo litaendelea hadi tarehe 4 Novemba 2026, ambapo Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 inatarajiwa kuzinduliwa rasmi.
Akifungua kongamano hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, huku zikihakikisha huduma zinazotolewa zinachochea ukuaji wa viwanda na biashara nchini.
Waziri Kapinga amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo kushirikiana na sekta binafsi, kutoa huduma kwa wakati na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima ili kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, WMA inaendelea kusimamia matumizi ya vipimo sahihi katika shughuli za uzalishaji na biashara ili kulinda maslahi ya walaji na wafanyabiashara, kuimarisha haki katika miamala na kuchangia maendeleo endelevu ya viwanda nchini.
Matumizi ya vipimo sahihi katika sekta ya viwanda yana umuhimu mkubwa katika kuhakikisha usahihi wa kiasi cha malighafi zinazotumika, bidhaa zinazozalishwa na zinazouzwa sokoni. Hatua hii husaidia kupunguza upotevu, kuongeza ufanisi wa uzalishaji na kujenga imani kati ya wazalishaji, wafanyabiashara na walaji.
Kupitia ushiriki wake katika kongamano hilo, WMA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi, wajasiriamali, wazalishaji na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kuzingatia matakwa ya kisheria katika matumizi ya vipimo pamoja na huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala.
Ushiriki wa WMA katika kongamano hili ni sehemu ya juhudi zake za kuhakikisha usimamizi wa vipimo unachangia kujenga mazingira ya biashara yenye haki, uwazi na ushindani, sambamba na malengo ya Serikali ya kukuza sekta ya viwanda na uchumi wa Taifa.
WMA inawakaribisha wananchi, wafanyabiashara, wajasiriamali, wazalishaji na wadau mbalimbali kutembelea banda lake katika maonesho hayo yanayoendelea hadi tarehe 4 Novemba 2026, ili kupata elimu na ufafanuzi kuhusu huduma za Wakala na umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo katika shughuli za kiuchumi.














0 Comments