Ticker

6/recent/ticker-posts

MADIWANI SIMANJIRO WASOMA TAARIFA ZA MIRADI YA MAENDELEO YA KATA ZAO

**************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamesoma taarifa mbalimbali za miradi ya maendeleo na changamoto zinazowakabili kwenye Kata zao 18.
Madiwani hao wamesoma taarifa za miradi hiyo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Baraka Kanunga Laizer, Makamu Mwenyekiti Sendeu Laizer na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Samwel Warioba.
Diwani wa Kata ya Edonyongijape, Jacob Kimeso amesema miongoni mwa mradi wa mafanikio kwenye Kata yake ni ujenzi wa shule mpya ya sekondari ambayo awali hawakuwa nayo.
Kimeso amesema wanafunzi wa eneo hilo wataanza kusoma kidato cha kwanza mwakani hivyo kuepukana na kutembelea umbali mrefu kufuata elimu.
Diwani wa Kata ya Terrat, Jackson Ole Materi amesema baadhi ya miradi ya maendeleo ni ya sekta ya afya, elimu na maji.
"Pamoja na hayo tunatarajia kujenga choo cha matundu 18 kwenye shule ya msingi Enongonoi ambapo awali wananchi walichangia fedha zao," amesema Ole Materi.
Diwani wa Kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi, amesema Kata yake ina shule moja ya sekondari Tanzanite na shule mbili za msingi za serikali.
Diwani wa Kata ya Naberera, Marco Munga amesema shule ya msingi Okutu imeongezewa madarasa mengine mapya.
Diwani wa viti maalum wa Tarafa ya Emboreet, Namnyak Edward akisoma taarifa ya Kata ya Loiborsiret amesema mafanikio yamepatikana kwenye sekta ya elimu.
Diwani wa Kata ya Shambarai, Julius Mamasita amesema miongoni mwa miradi mipya kwenye Kata yake ni ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Orbili itakayozinduliwa hivi karibuni. 

Post a Comment

0 Comments