Na Benny Mwaipaja, Bujumbura
MKUTANO wa 58 wa Magavana wa Afrika wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani IMF umemalizika Mjini Bujumbura nchini Burundi kwa kutoa msimamo wa pamoja wa kuziomba Taasisi hizo za fedha kuzijengea uwezo wa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano nchi za Afrika kwa ajili ya kuchochea uchumi wa nchi hizo.
Makubaliano mengine ya Magavana hao ni kuyaomba mashirika hayo ya fedha ya kimataifa kuzipatia nchi zao rasilimali fedha kwa ajili ya kukabiliana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia hususan katika suala la biashara ya mtandao, uchumi wa kidigitali na ujenzi wa miundombuni ya kidijitali ili kuifikia sehemu kubwa ya wananchi mijini na vijijini
Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, alisema kuwa msimamo huo wa pamoja umelenga kuwawezesha wananchi kuwa na uwezo wa kutumia teknolojia ya kidijitali katika kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii hususan katika kipindi hiki cha changamoto ya ugonjwa wa Uviko-19.
“Kizazi kilichoelimika kuhusu matumizi ya kidigitali, kinachangia maendeleo na kubuni nyenzo zinazosaidia kutekeleza kazi za ubunifu ili kukuza ajira na kuboresha maisha ya wananchi” Alisema Mhe. Masauni
Alizungumzia pia suala la umuhimu wa nchi za Afrika zenye vyanzo vya uhakika vya nishati ya umeme kujengewa uwezo na Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kufua umeme kutokana na vyanzo vya gharama nafuu kama maji na gesi asilia pamoja na kuhakikisha kuwa huduma hiyo ya umeme inawafikia wananchi wengi ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za kidigitali.
“Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watu wanaopata huduma ya nishati ya umeme barani Afrika imefikia chini ya asilimia mbili hivyo kuna umuhimu mkubwa wa Taasisi hizo za Fedha duniani kuzipatia nchi za Afrika rasilimali fedha kwa ajili ya miradi hiyo” Alisistiza Mhe. Masauni.
Mheshimiwa Masauni pia alisema kuwa, kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo ya umeme na miundombinu ya kidigitali, robo tatu ya wakazi bilioni 1.3 Barani Afrika hawatumii intaneti jambo linalokwaza wananchi kutumia fursa za kidijitali katika kuendesha maisha yao.
“Katika suala la umeme Tanzania tumepiga hatua kubwa ya usambazaji wa umeme vijijini kupitia Mradi wa REA lakini tunahitaji fedha zaidi kwa ajili ya kutekeleza miradi itakayochochea ukuaji wa uchuni na maendeleo ya watu katika nyanja ya matumizi ya dijitali, sekta ambayo hivi sasa ina ajiri idadi kubwa ya watu wakiwemo vijana na ni lazima miradi hiyo iwe ni ile yenye tija” Aliongeza Mhe. Masauni
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi za Kundi la Kwanza la Afrika Dkt. Taufila Nyamadzabo, alisema kuwa mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa na kuahidi kuwa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani IMF litayafanyiakazi kikamilifu maazimio yaliyofikiwa wakati wa Mikutano ya Taasisi hizo iliyopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2021, Washington, Marekani
“Kimsingi naamini Benki ya Dunia na IMF zitatoa fedha kwa nchi za Afrika katika kutimiza malengo yao ya kuwa na uwezo wa matumizi ya mifumo ya kidijiti, mifumo ya biashara ya mtandao pamoja na kuboresha nishati ya umeme lakini fedha hizo zitatolewa kwa kila nchi kivyake kadri zitakavyoomba kulingana na mahitaji na vigezo vinavyotakiwa” alisema Dkt. Nyamadzabo
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Burundi Dkt. Jilly Maleko alieleza kuwa Mkutano huo umefanyika muda muafaka kwa ajili ya mustakabali wa nchi za Afrika ambazo zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa kiuchumi kutokana na kusimama kwa shughuli nyingi za uzalishaji kwa sababu ya ugonjwa wa UVIKO-19.
“Wito wangu kwa Watanzania hasa vijana ni kuchangamkia fursa zitakazopatikana baada ya makubaliano yaliyofikiwa hapa kwa sababu katika kipindi hiki mifumo ya kidigitali kwa kutumia simu na kompyuta ndiyo inayotumika kwa kasi katika fursa mbalimbali za kujiletea maendeleo hivyo ni muhimu wakajifunza kikamilifu matumizi ya teknolojia hiyo” Alisema Dkt. Maleko
Mkutano wa 58 wa Magavana wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Dunia – IMF umezishirikisha nchi 54 za Bara la Afrika ambazo baadhi ya wajumbe walikuwepo katika Ukumbi wa Bunge la Burundi (Kigobe) mjini Bujumbura na wengine walishiriki kwa njia ya mtandao.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza kuhusu umuhimu wa Bara la Afrika kujengewa uwezo wa kuwa na vyanzo vya uhakika vya Umeme na kujenga miundombinu ya kidigitali, siku ya pili ya Mkutano wa Magavana wa Afrika wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani – IMF, Mjini Bujumbura Nchini Burundi. Kulia kwake ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Profesa Florens Luoga.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akifuatilia uwasilishwaji wa mada mbalimbali wakati wa Mkutano wa 58 wa Magavana wa Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF na Benki ya Dunia kutoka nchi 54 za Bara la Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Bunge la Burundi (Kigobe) mjini Bujumbura- Burundi.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Profesa Florens Luoga, akifuatilia mijadala kuhusu dhana ya Benki ya Dunia na IMF kuziwezesha nchi za Afrika kuwekeza kwenye TEHAMA ili kukuza uchumi wa nchi hizo wakati wa Mkutano wa 58 wa Magavana wa Benki ya Dunia Shirika la Fedha Duniani – IMF ulizishirikisha nchi 54 za Bara la Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Bunge la Burundi (Kigobe) mjini Bujumbura- Burundi.
Wataalam kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Nicolaus Shombe ambaye ni Kamishna wa Mipango ya Kitaifa (kushoto), Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uchambuzi wa Sera Bw. Yudica Saruni (katikati) na Kamishna Msaidizi Idara ya Fedha za Nje Bw. Robert Mtengule (kulia) wakisikiliza majadiliano ya Magavana wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha na Dunia-IMF kutoka nchi 54 za Afrika, uliofanyika mjini Bujumbura-Burundi.
Mshauri Mwandamizi wa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Afrika Dkt. Zarau Kibwe, akifuatilia matukio wakati wa Mkutano wa 58 wa Magavana wa Afrika wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani– IMF, uliofanyika katika Ukumbi wa Bunge la Burundi (Kigobe) mjini Bujumbura.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anayesimamia masuala ya Fedha za Nje Bi. Amina Khamis Shaaban na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar Bw. Aboud Hassan Mwinyi, wakiwa katika Mkutano wa 58 wa Magavana wa Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF na Benki ya Dunia uliomalizika mjini Bujumbura-Burundi.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango, Bujumbura)
0 Comments