Na Mwandishi Wetu- Mwanza
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza Mhe, Mary Masanja leo ametoa msaada wa shilingi laki 2 kwa mtoto Shamsa Ramadhan Yusuph (9) ambaye alikua anaishi katika mazingira magumu katika Kata ya Isamilo, Halmashauri ya Jiji la Mwanza kabla ya kuchukuliwa na Mkurugenzi wa Nitetee Foundation, Dkt. Flora Lauwo.
Mhe. Masanja ametoa msaada kwa mtoto huyo kufuatia taarifa zilizochapishwa katika mitandao ya kijamii na Mkurugenzi wa Nitetee Foundation, Dkt. Flora Lauwo, kuhusu hali ngumu ya maisha ya mtoto huyo.
Mhe. Masanja amesema fedha hizo zisaidie katika kununua vifaa vya shule kama madaftari, kalamu, n.k.
“Nakukabidhi fedha hizi kidogo zikusaidie kununua vifaa vya shule”Mhe. Masanja amesema.
Ameongeza kuwa, ataendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mtoto huyo ikiwemo kuhakikisha anahudhuria masomo na kufuatilia afya yake na ya bibi yake.
Aidha, Mhe. Masanja amewashukuru Waheshimiwa Wabunge wanawake kwa kufuatilia suala hilo la mtoto ambaye amegusa hisia kwa Wazazi/walezi wengi wanaofuatilia habari kama hizi.
Pia, amewapongeza Watanzania wote wenye moyo wa kujitoa kwa ajili ya wengine.
Naye, Mkurugenzi wa Nitetee Foundation, Dkt. Flora Lauwo ameishukuru Serikali kwa jitihada zinazoifanya kuhakikisha Shamsa anasoma na anaendelea kupata matibabu .
“Ninatoa shuktrani zangu za dhati kwa Serikali kwa kuliona tatizo hili na sasa mtoto amepata shule na tutaanza rasmi kushughulikia taratibu za shule na nitawarudia kuwaambia kinachoendelea” Dkt. Lauwo amesema.
Kwa upande wake Shamsa Yusuph amesema anapenda kusoma shule hivyo amewaomba watanzania wamsaidie ili apate fedha za kumuwezesha kwenda shule.
Aidha, amewaomba watanzania kumsaidia fedha za matibabu kwa ajili kwa ajili ya bibi yake ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.
Mhe. Mary Masanja kama Mbunge wa Viti Maalum Mwanza yupo Mkoani hapo kwa ajili ya kutembelea kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu Wilayani Magu, kukutana na Baraza la UWT Wilaya ya Magu, Nyamagana, Ilemela, Kwimba, Ukerewe, Misungwi na Sengerema.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, Mhe, Mary Masanja (katikati) akizungumza na mtoto Shamsa Ramadhan Yusuph (9) (kushoto) ambaye anaishi katika mazingira magumu baada ya kumtembelea katika Jiji la Mwanza leo. Anayeshuhudia ni Mkurugenzi wa Nitetee Foundation, Dkt. Flora Lauwo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, Mhe, Mary Masanja akimkabidhi msaada wa fedha kiasi cha shilingi laki 2 mtoto Shamsa Ramadhan Yusuph (9) (katikati) ambaye anaishi katika mazingira magumu baada ya kumtembelea katika Jiji la Mwanza leo. Anayeshuhudia ni Mkurugenzi wa Nitetee Foundation, Dkt. Flora Lauwo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, Mhe, Mary Masanja (kushoto) akizungumza na mtoto Shamsa Ramadhan Yusuph (9) (katikati) ambaye anaishi katika mazingira magumu baada ya kumtembelea katika Jiji la Mwanza leo. Anayeshuhudia ni Mkurugenzi wa Nitetee Foundation, Dkt. Flora Lauwo.
0 Comments