Ticker

6/recent/ticker-posts

WAFUGAJI WAJENGEWA USTAHIMILIVU WA MABADILIKO YA TABIANCHI KWA MTAZAMO WA KIJINSIA

 

Na Deogratius Koyanga, Njombe

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia Mradi wa “Ustahimilivu Wao, Dunia Yetu” umeendesha mafunzo kwa wafugaji kutoka kata nne za Igima, Igwachanya, Usuka na Iturahumba, kwa lengo la kujenga uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na ushirikishwaji wa makundi yote.

Mafunzo hayo yaliwakutanisha wafugaji wa asili na wale wanaotumia mifumo ya kisasa ya ufugaji, yakilenga kuwajengea uwezo wa kuwashirikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika maamuzi yanayohusu rasilimali za ufugaji, ili kuepuka makundi hayo kuathirika zaidi na changamoto za tabianchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo, mwezeshaji kutoka TGNP, Deogratius Temba, alisema mabadiliko ya tabianchi yanaongeza mzigo mkubwa kwa wanawake katika jamii za wafugaji.

“Wanawake ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Wanatembea umbali mrefu kutafuta maji, watoto hukosa masomo na ukatili wa kijinsia huongezeka. Ndiyo maana ni lazima washirikishwe katika kila uamuzi wa kifamilia na kikundi,” alisema Temba.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walisema elimu waliyoipata itabadilisha namna wanavyofanya maamuzi katika ngazi ya familia.
 Christopher Msigwa kutoka Kijiji cha Indilamunyo alisema kuwa kushirikisha wenza wao kutasaidia kuokoa mifugo hasa nyakati za ukame.
“Maamuzi ya pamoja yatatusaidia kulinda mifugo na ustawi wa familia wakati wa mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Naye Fadhili Mangula kutoka Kata ya Igima alibainisha kuwa usawa wa kijinsia utaimarisha uwajibikaji katika ufugaji, huku Michael Mlowe wa Kijiji cha Mlevela na Peter Kiswaga wa Kata ya Usuka wakisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira.

Washiriki hao walikubaliana kuzuia ukataji miti hovyo, kulinda vyanzo vya maji, kupanda miti na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa jamii, kama sehemu ya kujenga ustahimilivu wa muda mrefu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mradi wa “Ustahimilivu Wao, Dunia Yetu” unaotekelezwa kwa ushirikiano na CARE Tanzania pamoja na mashirika mengine unaendelea kuchochea mabadiliko chanya katika jamii za wafugaji kwa kuweka mbele ushirikishwaji, haki na usawa wa kijinsia.

Post a Comment

0 Comments