WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 300 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa makao makuu ya nchi jijini Dodoma.
“Rais Mheshimiwa Samia Suluhu, amedhamiria kuendeleza miradi yote ikiwemo ya ujenzi wa makao makuu na miradi mbalimbali inayofanyika hapa Dodoma. Hatua hii ni uthibitisho tosha kwa Watanzania kuwa kazi zinaendelea.”
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Agosti 13, 2021) baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Ikulu mpya Chamwino, Dodoma ambao umefikia asilimia 78.
“Ujenzi wa Makao Makuu bado unaendelea, Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza kazi zote ziendelee zikiwemo za ujenzi wa mji wa Serikali hapa Dodoma.”
Amesema kuwa kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 131 zitatumika katika ujenzi wa majengo ya magorofa ya makao makuu ya wizara kwenye Mji wa Serikali, Mtumba.
Aidha, Waziri Mkuu amesema shilingi bilioni 169 zitapelekwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya maboresho ya jiji hilo ikiwemo miundombinu ya barabara, maji na umeme.
Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama akutane na Mawaziri wenzake ili waanze mchakato wa ujenzi majengo ya wizara. “Ujenzi huo unatakiwa uanze Septemba, mwaka huu na ufanywe na kampuni za ukandarasi za Serikali pamoja na kampuni za sekta binafsi,” amesema.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na viwango vya ujenzi wa mradi huo na hatua iliyofikiwa na kwamba ana imani utakamilika kwa wakati.
“Leo nimefarijika kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi huu na furaha hii inatokana na hatua tuliyoanzia na tulipofikia sasa. Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alitaka kuona Ikulu mpya inafanana na ya Dar es Salaam na leo nimeona kweli zinafanana.”
Jengo la Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma linalojengwa na SUMA JKT ambalo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua ujenzi wake, Agosti 13, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na vijana wa SUMA JKT baada ya kukagua ujenzi wa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Agosti 13, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Agosti 13, 2021. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Agosti 13, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
0 Comments