Ticker

6/recent/ticker-posts

RC SENGATI AITAKA WIZARA YA NISHATI KUIWEZESHA KAHAMA KUJITEGEMEA KINISHATI

Na Anthony Ishengoma –Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati ameiomba Wizara ya Nishati kuifanya Kahama kuwa sehemu inayojitegemea kinishati tofauti na ilivyo sasa ambapo imeunganishwa na TANESCO Mkoa kutokana na umuhimu wake katika pato la Taifa na uwekezaji katika viwanda unaohitaji nishati ya kutosha ya umeme.

Dkt. Sengati aliongeza kuwa kwa Mkoa mzima wa Shinyanga bili ya umeme inayoenda TANESCO ni kiasi cha Shilingi Bil.8 kwa mwezi na kati ya hizo Kahama inalipa kiasi cha Shilingi Bil.7 suala linaloonesha uwezo mkubwa wa kiuchumi kwa Kahama na uwekezaji ulioko Kahama.

Dr. Sengati alisema hayo jana alipofanya ziara ya siku moja katika Manispaa hiyo Kahama na kutembelea eneo la uwekezaji la Chapulwa ambapo kuna ujenzi wa viwanda vitatu vya kusindika vinywaji, nafaka na dawa vinavyojengwa na kampuni ya Kahama Oil Kom kwa uwekezaji wa zaidi Bil.200.

‘’Hapa tunachangamoto ya umeme na tunategemea kiwanda kimojawapo hapa kuanza kuzalisha vinywaji mwezi Januari lakini hatujawa na uhakika wa umeme kwenye uwekezaji huu wenye thamani zaidi ya Bil 200.’’Aliongeza Dkt. Philemon Sengati Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Dkt. Sengati aliuhakikishia uongozi wa Wilaya ya Kahama kuwa ataendelea kuwasiliana na Wizara ya Nishati hasa Waziri wa Nishati Medard Kalemani kuona umuhimu wa kuwa na mikoa miwili Kitanesco kwasababu uwekezaji Kahama ni mkubwa na ni eneo linalokuwa kiviwanda.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Bw. Anderson Nsumba alisema kuwa Manispaa ya Kahama inatoa ardhi bure kwa mwekezaji ambaye ana nia ya kweli ya kuwekeza lakini ukionesha una mashaka katika uwekezaji Manispaa inakutoza kiasi cha Shilingi Mil.2 kwa kila eka ili uweze kupata msukumo katika kuwekeza.

Bw. Nsumba aliongeza kuwa Manispa yake ina jumla ya eka elfu sita kwa ajili ya uwekezaji na katika izo tayari imetoa eka 90 kwa mwekezaji wa Kahama Oil Kom ambaye tayari ameanza ujenzi wa Viwanda katika eneo hilo.

Aidha Kiongozi huyo wa Manispaa ya Kahama amesema tayari ameisha toa eneo kwa kampuni ya GSM lenye ukubwa wa eka 40 ambayo tayari imelipa fidia wananchi na kampuni moja toka Sudani eka 60 pamoja na mwekezaji katika kiwanda cha Simenti ambao wote wamevutiwa kuwekeza katika eneo la Chapulwa.

Bw. Nsumba aliwataka kuwekeza Kahama kutokana na uwepo wa fursa akiitaja Kahama yenyewe kuwa fursa kwani yenyewe ni lango la biashara kwa kupakana na Nchi za Maziwa Makuu lakini pia uwepowa idadi kubwa ya watu katika kanda ya ziwa ambao peke yake ni soko la kutosha kwa wewekezeji kupata fursa ya kibiashara.

Naye Meneja Uzalishaji wa kampuni ya Kahama Oil Kom amesema kiwanda cha usindikaji kitaanza uzalishaji mwezi Januari kitakuwa na uwezo wa kuzalisha chupa elfu 32 kwa saa lakini pia vinywaji vingine kama juice zitazalishwa kwa kiwango kilekile kwa saa.

Pamoja na ziara yake katika eneo hilo la uwekezaji Mkuu wa Mkoa pia litembelea maeneo mengine ya mji huo kwa lengo la kujionea maendeleo ya biashara katika Manispaa ya Kahama ikiwemo kujiweka tayari kupokea Mkutano mkubwa wa tathimini ya lishe utakofanyika Kitaifa katika Manispaa hiyo tarehe 26 na 27 Mwezi huu.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dr. Philemon Sengati katikati pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bi. Zuena Omary kulia kwake akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kituo cha Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kilichopo Manispaa ya Kahama jana alipofika Kituoni hapo wakati wa ziara yake kujionea shughuli za maendeleo katika Manispaa hiyo.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dr. Philemon Sengati wa kwanza kushoto pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bi. Zuena Omary wa kwanza kushoto na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Bw. Anderson Nsumba wakishauliana jambo wakati wa ziara yake kujionea shughuli za maendeleo katika Manispaa hiyo.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dr. Philemon Sengati akiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bi. Zuena Omary wakiwa wameongozana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Bw. Anderson Nsumba wakishauliana mambo tofauti wakati wa ziara yake kujionea shughuli za maendeleo katika Manispaa hiyo.

Post a Comment

0 Comments