Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI SILINDE AZIAGIZA HALMASHAURI KUHAKIKISHA WANAKUWA NA TAKWIMU SAHIHI KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUMU

Na Asila Twaha-TAMISEMI


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. David Silinde ameziagiza, Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanakuwa na takwimu sahihi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili wanafunzi hao wapatiwa huduma sawa na wanafunzi wengine.  


Akizungumza mbele wajumbe wa Umoja wa Maafisa Elimu Elimu Maalum (UMEMTA) Agosti 23, 2021 Jijini Dodoma akifungua kikao cha kwanza kilichowakutanisha Maafisa  hao  wa Halmashauri 184  Tanzania Bara kwa lengo la kujadili  mambo muhimu yahusuyo elimu maalum nchini. 


Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuhakikisha suala la kuwatambua wanafunzi wenye mahitaji maalumu ni kipaumbele  sawa na wanafunzi wengine kwa kuboresha miundombinu  pamoja na kuajiri walimu wakuwafundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum.


Silinde amesema mpaka mwezi Januari, 2021 zaidi ya watoto 28,698 wamebainishwa kuwa na  mahitaji maalum aidha kiasi  cha shilingi bilioni 4.5 zimetumika kununulia vifaa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.



‘’Naagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa ikasimamie na kusambaza vifaa vilivyonunuliwa ili viwafikie walengwa na vitumika kama vilivyokusudiwa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum’’ amesema Silinde.


Aidha amewaagiza maafisa elimu maalumu kutoa elimu kwa jamii kwa kutowatenga, kutowanyanyapapa na kuwabaini  wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kushirikiana na serikali kwa pamoja na kuwapatia haki sawa na wanafunzi wengine katika elimu. 


Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Maafisa Elimu Elimu Maalum  Bw. Joshua Samson ameishukuru  Serikali kwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi  kwa kuendelea kutoa  kipaumbele katika masuala mbalimbali yakiwemo elimu, ajira, uteuzi na ujenzi wa miundombinu rafiki pamoja na huduma za Afya. 


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. David Silinde akikagua Maonesho yalikwenda sambamba na Mkutano huo katika Viwanja vya Chuo cha Mipango.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. David Silinde akifungua kikao cha kwanza kilichowakutanisha Maafisa Elimu Elimu Maalum (UMEMTA) Agosti 23, 2021 Jijini Dodoma.



Baadhi ya Washiriki wa Mkutano huo.

Post a Comment

0 Comments