UCHAMBUZI WA KIJINSIA WA TEUZI ZA RAIS
MH. SAMIA SULUHU HASSAN KATIKA NAFASI ZA WAKURUGENZI WATENDAJI WA HALMASHAURI ZA JIJI, MANISPAA, MIJI NA WILAYA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi, utenguzi na kuwabadirisha vituo vya kazi Wakurugenzi Watendaji wa Jiji, Manispaa, Miji na Wilaya katika Halmashauri mbalimbali hapa nchini mnamo tarehe 1 Agosti 2021.
Katika uteuzi huu, wakurugenzi wapya 69 wamewateuliwa, ambapo wanawake walikuwa 33 (48%) na wanaume 36 (52%). Katika hao, 15 wamejaza nafasi zilizokuwa wazi na 54 wamechukua nafasi za waliotenguliwa.
Hii inafanya kuwe na
jumla ya wakurugenzi wanawake 55 sawa na asilimia 29 ya wakurugenzi wote 184 wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.
Hili ni ongezeko la asimilia 11
ikilinganishwa na idadi ya wakurugenzi 33 (18%) kati ya 185 walioteuliwa katika
awamu ya tano huku wanaume wakiongoza kwa 82% (152).
Mhe. Rais pia amewahamisha Wakurugenzi 70 na kuwaacha wakurugenzi 45 wa zamani kwenye vituo vyao vya kazi.
Uteuzi huu umefanya idadi ya viongozi wanawake
aliowateua Rais Samia Suluhu Hassan tangu aapishwe rasmi Machi 19, 2021 kuwa Rais wa awamu ya sita katika Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kufikia 144
sawa na 31% na wanaume kufikia 317 sawa na 69% ya
wateuliwa wote 461.
TGNP kama taasisi kinara katika kutetea Haki za Wanawake, ikiwemo kupigania ongezeko la idadi ya wanawake kwenye nafasi za uongozi katika vyombo mbalimbali vya maamuzi, tunapongeza jitihada hizi za maksudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, sambamba na kuwasihi viongozi wote waliopewa dhamana katika nafasi mbalimbali kutambua kuwa hatma ya Watanzania hususani wanawake ambao wengi hawako katika ajira rasmi, wana mitaji midogo na hawana ujuzi stahiki wa kufaidika na rasilimali za nchi kama vile madini, mafuta na gesi, ziko mikononi mwa maamuzi yanayofanywa na viongozi hao.
Sambamba na hilo, TGNP inatambua kuwa Amani na Utulivu ni mambo ya msingi katika kufikia usawa wa kijinsia, maendeleo endelevu na jumuishi.
Hivyo, tunatoa wito kwa wadau wote ikiwemo Serikali, Viongozi wa
Dini, Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi kukaa pamoja na kujadiliana
juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Taifa letu kwa faida ya Watanzania walio
wengi na makundi mengine yaliyoko pembezoni.
TGNP, inatoa pia wito kwa mamlaka za teuzi kutoa
taarifa za teuzi hizo kijinsia kwa kuchanganua wazi taarifa kama vile jinsi za
wateule ili kuepusha mkanganyiko kwa watumiaji wa taarifa hizi.
Sambamba na hilo, TGNP itaendelea kushirikiana na
Serikali ya Awamu ya Sita kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia kutoa mapendekezo
yanayopelekea kufikiwa kwa haraka usawa wa kijinsia katika Taifa letu.
Imetolewa na:
Mtandao
wa Jinsia Tanzania (TGNP)
0 Comments