Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, amemuagiza Mtendaji Mkuu mpya wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila, kuhakikisha anatatua changamoto mbalimbali zinazozikabili wakala huo, ili kuendeleza heshima iliyojijengea kwa wadau wake hapa nchini na kimataifa.
Waziri huyo alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kumkabidhi ofisi Mtendaji Mkuu huyo, ambapo pamoja na mambo mengine alimtaka kuhakikisha kuwa anasimamia vema mtandao wa barabara nchini wenye jumla ya urefu wa kilometa 36,000.
"TANROADS inasimamia ujenzi wa barabara hizi kwa kiwango cha lami, ujenzi wa madaraja na matengenezo ya barabara, hivyo hakikisheni zinapitika muda wote, pamoja na kuhakikisha magari yanayopita katika barabara hizi hayazidishi uzito kwa kusimamia vyema mizani zote nchini," alisema Dk. Chamuriho.
Mbali na hilo, Dkt. Chamuriho, aliwasisitiza pia kuhakikisha wanapunguza malalamiko mbalimbali ikiwamo ucheleweshaji wa miradi inayosababishwa na kuchelewa kwa misamaha ya kodi, ujenzi wa barabara chini ya kiwango na ucheleweshaji wa malipo ya fidia kwa wananchi wenye haki ya kulipwa ambao wanapisha miradi mbalimbali ya ujenzi inayosimamiwa na Wakala huo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila. alimhakikishia Waziri Chamuriho kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kutoa ushirikiano kwa watumishi waliopo chini yake, kwani amekuwa katika sekta hiyo kwa muda mrefu, hivyo anazifahamu changamoto zote zilizopo.
"Niwatake watumishi wenzangu kujitathimini na kutokusubiri kutathiminiwa pamoja na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ili kuendeleza Taasisi hii muhimu nchini katika kukuza uchumi wa Taifa”, alisema Mativila.
Shughuli hiyo ya makabidhiano ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Malongo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Raphael Nombo, Wajumbe wa Bodi ya TANROADS pamoja na Manejimenti ya TANROADS.
Mtendaji Mkuu huyo alikabidhiwa nyaraka mbalimbali zikiwamo muundo wa Wakala, Sheria, Kanuni na Sera mbalimbali pamoja na Bajeti ya TANROADS ili ziweze kumuongoza katika majukumu yake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Aliyekuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Crispianus Ako, akimkabidhi nyaraka Mtendaji Mkuu Mpya wa Wakala huo, Mhandisi Rogatus Mativila, leo jijini Dar es Salaam. Mhandisi Rogatus Mativila ameziba nafasi ya aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Hayati Patrick Mfugale.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho (wa tatu kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Wizara, wajumbe wa Bodi na Watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wakati wa hafla ya kumkabidhi ofisi Mtendaji Mkuu Mpya wa Wakala huo, Mhandisi Rogatus Mativila, jijini Dar es Salaam.
0 Comments