Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AKAGUA MRADI WA KITUO CHA HUDUMA YA PAMOJA MPAKANI


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akikagua mradi wa ujenzi wa kituo cha huduma ya pamoja mpakani wilayani Kyela, Mkoa wa Mbeya hivi karibuni

NA MWANDISHI WETU

 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amefanya ziara ya kikazi mkoani Mbeya ambapo pamoja na mambo mengine ametembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha huduma ya pamoja mpakani eneo la Kasumulu/Songwe katika mpaka wa Tanzania na Malawi (OSBP). 

Mradi huo unatekelezwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), huku ujenzi wake ukihusisha awamu tatu ambapo kwa sasa ni awamu ya kwanza na pili. 

Akiwa katika mradi huo Mhe. Majaliwa ametaka kuwekwe miundombinu itakayotoa fursa kwa wajasiriamali wa eneo husika kufanya biashara, hivyo ameagiza kujengwe kituo cha mabasi. 

"Nimekuja kuona kama miundombinu inatosheleza na isitoshe tu kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini, bali itosheleze pia kwa wenyeji wa eneo hili, wafanye biashara na hivyo ni lazima kijengwe kituo cha Mabasi," amesema.

Waziri Mkuu, amesema suala la ujenzi wa kituo hicho cha mabasi lipo chini ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela na Baraza lake la Madiwani, ambapo wanapaswa kutafuta eneo kwani kituo hicho kitainufaisha halmashauri yao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amesema awamu ya kwanza na ya pili ya mradi huo imegharimu sh. bilioni 26.4 huku ya tatu itagharimu sh. bilioni 14.2.

Ameuagiza Wakala wa Barabara a Tanzania (TANROADS), baada ya kukamilika kwa mradi huo kutenga eneo litakalokuwa kivutio ili machinga na mamalishe wanufaike. 

Akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Eliazary Rweikiza, amesema mradi huo unatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB).

Kwa mujibu wa mhandisi Rweikiza, mkandarasi wa mradi huo ni Kampuni ya China Geo Engineering Corporation (CGEC) kutoka nchini China na msimamizi ni ECG Engineering Consultant Group S.A ya Misri kwa kushirikina na Wakala wa Majengo (TBA).

Amesema mkataba wa ujenzi ulisainiwa Juni 12 mwaka 2019 na kazi zilianza Oktoba mosi mwaka huo na unatarajiwa kukamilika Septemba 30, mwaka huu.     

Amezitaja gharama za mkataba ukihusisha na kodi ya ongezeko la thamanmi ni sh. bilioni 26.426, huku gharama za ushauri ni dola za Marekani 443,675.

Mhandisi Rweikiza amesema katika awamu ya kwanza kazi zilizofanywa ni ujenzi wa majengo tisa, kazi za nje na miundombinu kadhaa ambayo ni Jengo la abiria, jengo la malori, Ghala, geti namba moja, geti namba mbili na jengo la mifugo.

Ametaja mengine ni jengo la kupima uzito, jengo la maegesho namba moja na mbili.

Kuhusu kazi za nje zilizofanywa amesema ni barabara zenye urefu wa kilometa 2.56, uzio wenye urefu wa kilometa 2.2, mfumo wa maji safi, mwa maji taka, kazi za umeme, mizani ya kupima uzito magari, kuboresha mazingira na maegesho ya magari.

Amesema katika awamu hiyo, nyingine zilizofanywa ni ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo matenki ya ardhini ya kuhifadhia maji, matenki ya maji taka na mifumo ya mawasiliano ya habari.

Ameitaja mingine ni mifumo ya kamera za ulinzi na tahadhari (CCTV, Fire alarm systems, Access control systems), mifumo ya kazi za umeme, mifumo ya kupambana na moto na mifumo ya kupooza joto.

Katika awamu ya tatu, amesema kazi zilizopangwa kufanywa ni ujenzi wa jengo la huduma za ujenzi, jengo la huduma, kituo cha zima moto na matanki ya umwagiliaji namba moja na mbili.

Amebainisha kuwa kazi hizo hazipo katika mkataba unaondelea na maombi ya fedha zake ambazo ni sh. bilioni 14.169, yameshawasilishwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa ajili ya utekelezaji.

Amesema kufikia mwishoni mwa Julai mwaka huu, Mkandarasi alishalipwa madai yote ambayo ni zaidi ya sh. bilioni 13.994 huku malipo ya fidia kupisha ujenzi yakiwa ni zaidi ya sh. bilioni 5.779 na tayari yameshalipwa.

Amesema kutokana na mkataba mradi ulipangwa kukamilika Septemba 30, mwaka jana na mkandarasi aliomba nyongeza ya muda hivyo kazi itakamilika September mwaka huu.

Ameeleza kufikia Julai 31, mwaka huu kazi zilikuwa zimekamilika kw wastani wa asilimia 67.

Amesema jengo la malori limefikia asilimia 78, ghala asilimia 80, jengo la mifugo asilimia 85, jengo la abiria asilimia 80, geti namba moja na mbili yamefikia asilimia 75, Mizani asilimia 85 na ‘Steel shed namba mbili asilimia 70.

Ameitaja miradi mingine ni tanki kuu la kuhifadhi maji asilimia 80, kazi nje na za barabara zimefikia asilimia 43, ofisi za wahandisi na maabara imekamilika kwa asilimia 100.

Post a Comment

0 Comments