Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imekutana na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Shinyanga kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) katika kikao kazi kilicholenga kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano na kuboresha utoaji wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira kwa wananchi.
Kikao hicho kimefanyika leo Jumamosi Machi 14, 2026 mjini Shinyanga na kuongozwa na Mkurugenzi wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, ambaye ametumia fursa hiyo kueleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na mamlaka hiyo kuboresha huduma za maji katika mkoa huo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Katopola amesema SHUWASA inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma za usambazaji wa maji kwa wananchi, ikiwemo kuimarisha miundombinu ya maji, kupanua mtandao wa usambazaji ili kufikia maeneo ambayo hayakuwa na huduma hiyo, pamoja na kushughulikia changamoto ndogondogo zinazojitokeza katika utoaji wa huduma.
Amebainisha kuwa ushirikiano kati ya SHUWASA na vyombo vya habari una mchango mkubwa katika kuwafikishia wananchi taarifa sahihi kuhusu huduma za maji, miradi inayotekelezwa pamoja na changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.
“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya maji, kulinda miundombinu ya maji pamoja na kusaidia kufikisha maoni na changamoto za wananchi ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati,” amesema Katopola.
Aidha amewaomba waandishi wa habari kuendelea kuwahabarisha wananchi kuhusu juhudi zinazofanywa na SHUWASA katika kuhakikisha wanapata huduma za uhakika za maji, ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu majukumu na kazi zinazofanywa na mamlaka hiyo.
Kwa upande wao, waandishi wa habari waliohudhuria kikao hicho wameahidi kuendelea kushirikiana na SHUWASA katika kuhabarisha umma kuhusu masuala ya maji, wakieleza kuwa taarifa sahihi na kwa wakati zitasaidia kuongeza uelewa wa wananchi.
Pia wametoa ushauri mbalimbali utakaosaidia kuimarisha zaidi utoaji wa huduma za maji kwa jamii, wakisisitiza kuwa suala la maji ni hitaji muhimu kwa maisha ya wananchi na maendeleo ya jamii.


Mkurugenzi wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola.



































































0 Comments