Ticker

6/recent/ticker-posts

MHE.MCHENGERWA-WATUMISHI WA UMMA WATAKAOPIGWA SIMU NA MATAPELI WATOE TAARIFA TCRA KWA NAMBA YA SIMU 15040


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) leo Jijini Dar es Salaam. (PICHA NA EMMANUEL MBATILO)

******************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewatahadharisha Watumishi wa Umma, Watumishi wastaafu na wananchi kwa ujumla kutokutoa fedha au taarifa zao kwa watu ambao wanakithiwa kuwa ni matapeli hivyo kuwataka kutoa taarifa katika ofisi husika ili waweze kushughulikiwa.

Mhe.Mchengerwa amesema hayo leo alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) leo Jijini Dar es Salaam.

Aidha Mhe.Mchengerwa ametoa onyo kwa wale wote ambao wanajihusisha na uhalifu huo kuacha mara moja kwani Serikali kupitia vyombo vyake inaendelea kufuatilia taarifa hizo kwa ukaribu ili kuweza kuwabaini matapeli hao.

"Niwaombe Watumishi wa Umma na wananchi kwa ujumla wenye taarifa za mtu yeyote wakiwemo Watumishi wa Umma wanaojihusisha na vitendo vya kiharifu vya namna hii kuleta taarifa zao sehemu husika". Amesema Waziri Mchengerwa.

Amesema Watumishi wa Umma watakaopigiwa simu na matapeli na kuombwa kutoa fedha au taarifa zao ili waweze kushughulikiwa masuala yao wawasilishe namba za simu zilizotumiwa na waharifu hao katika Mamlaka za Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia namba ya simu 15040.

Sambamba na hayo Waziri Mchengerwa amewataarifu wananchi na Watumishi wa Umma kuwa endapo watahitaji ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya kiutumishi wapige simu katika kituo cha mawasiliano cha ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa namba ya simu 0262160240 au kwenye kituo cha mawasiliano cha Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia namba ya simu 0262160210.

Hata hivyo Mhe.Mchengerwa amewataka watumishi wa Umma katika maeneo yao ya kazi kuhakikisha wanaondosha urasimu na kutoa nafasi ya kuwasikiliza wananchi kero zao.

"Niwaombe viongozi walioteuliwa na kuchaguliwa wawasikilize wananchi na kuweza kutatua kero zao na kuepusha urasimu katika ofisi zao ili kutoa fursa kwa watanzania kupeleka kero zao na malalamiko yao waweze kuwasikiliza na kupata ufumbuzi kuhusu kero zao kwani ongezeko la urasimu popote mahala pa kazi hutengeneza mazingira ya kiutapeli na kutoa nafasi kwa watu wasio wema kutumia fursa hiyo kufanya utapeli kwa Watumishi na wananchi kwa ujumla katika mazingira yao". Amesema Mhe.Mchengerwa.

Post a Comment

0 Comments