Ticker

6/recent/ticker-posts

VIJANA RUKWA WAANZISHA MIRADI YA LISHE ENDELEVU

Mkoa wa Rukwa licha ya kuwa ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula bado unakabiliwa na tatizo la udumavu unaotokana na lishe duni hivyo serikali na wadau wamebuni miradi ya lishe bora kupitia kilimo na ufugaji.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa mradi wa Lishe Endelevu chini ya Shirika la Save The Children Rukwa Emanuel Magoyo wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Mkoa iliyotembelea mashamba darasa, ufugaji kuku, sungura na samaki kwenye wilaya za Sumbawanga na Nkasi mwishoni mwa wiki hii.

Magoyo alisema mradi umefanikiwa kufundisha vijana zaidi ya 700 na maafisa ugani 187 toka wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo kutekeleza miradi ya lishe bora hatua inayosaidia kuondoa tatizo la udumavu linaloathiri zaidi watoto wadogo.

“Mradi umefankiwa kutoa mafunzo juu ya lishe bora, teknolojia ya umwagiliaji, kutoa mbegu bora za mazao ya mboga mboga, matunda na vifaranga vya kuku bora na samaki ili vijana na akina mama wanzishe miradi ya lishe bora “alisema Magoyo.

Kamati pia ilitembelea shamba darasa la kijana Morgan Yiskaka wa kijiji cha Milundikwa wilaya ya Nkasi ambaye amefanikiwa kuzalisha aina 12 za mazao ya mboga mboga na ufugaji samaki ikiwa ni mkakati wa kuboresha lishe endelevu kwenye jamii.

Akizungumzia mafanikio aliyoyapata chini ya mradi wa lishe endelevu Yiskaka alisema tangu mwaka 2017 vijana na akina mama wengi wamepata mafunzo ya kilimo bora toka shambani hapo chini ya uratibu wa Save The Children.

“Hapa ninazalisha mazao zaidi ya 12 mchanganyiko ili kuchochea upatikanaji wa lishe bora katika jamii. Sasa nina soko kubwa la mazao ya mboga mboga kutokana na watu wengi kutambua faida zake kwa afya” alisema kijana Yiskaka.

Naye Mratibu wa Lishe Mkoa wa Rukwa Teddy Swallo alisema tafiti za mwaka 2018 za Wizara ya Afya zinaonesha tatizo la udumavu liko takribani asilimia 47 kwa mkoa wa Rukwa hivyo kuhitaji mikakati ya kuliondoa kupitia miradi ya lishe endelevu ikiwemo kilimo cha mboga mboga na ufugaji” alisema Swallo.

Swallo alibainisha kuwa mradi wa lishe endelevu kwenye mkoa wa Rukwa unalenga kuboresha hali ya lishe kwa akina mama wajawazito, watoto wadogo na vijana ili waweze kubadili tabia za ulaji chakula bora.

“Pamoja na kuwa na elimu ya ufugaji au kilimo cha mboga mboga ni budi tukabadili tabia zetu za kula ikiwemo kupata mlo kamili kwa makundi yote matano ya nafaka, wanyama, mboga mboga, matunda na mafuta” alisisitiza Swallo.

Mratibu huyo alitaja madhara ya udumavu kwa watoto kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo mdogo wa kufikiri (akili) na kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata maradhi mbalimbali.

Akizungumzia juu ya mradi wa ufugaji kuku bora Mkulima Kiongozi wa kijiji cha Mkangale Namanyele Elizabeth Ngalawa alisema wanashauri wakulima wasipige mahindi dawa zisizo na ubora ili kutoathiri chakula cha binadamu na mifugo.

Aliongeza kusema kikundi chao kinajihusisha na ufugaji bora wa kuku aina na Saso pamoja na shamba kilimo ili kujenga tabia ya kula lishe bora ikiwemo kukuza kipato cha kaya baada ya kupata mafunzo toka wataalam wa mradi wa USAID/Lishe Endelevu.

Mwisho.

Imeandaliwa na;

Afisa Habari Mkuu,

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa

SUMBAWANGA

05.09.2021

Wajumbe wa Kamati ya Lishe Mkoa wa Rukwa wakiwa shule ya sekondari Nkasi kutembelea mradi wa ufugaji sungura unaotekelezwa na wanafunzi kwa ajili ya kuboresha lishe bora.

Kijana Morgan Yiskaka akitoa maelezo kuhusu shamba darasa la mboga mboga linalotumika kufundisha vijana juu ya lishe bora chini ya shirika la USAID/Lishe Endelevu kijiji cha Milundikwa wilaya ya Nkasi .

Mkulima Kiongozi Elizabeth Ngalawa (wa kwanza kushoto) akiwa na wana kikundi wenzake wa ufugaji kuku bora aina ya Saso kijiji cha Mkalange wilaya ya Nkasi wakati walipotembelewa na Wajumbe wa Kamati ya Lishe Mkoa wa Rukwa kukagua mradi huo.

Wajumbe wa Kamati ya Lishe Mkoa wa Rukwa wakikagua mradi wa shamba darasa la mboga mboga na ufugaji samaki kijiji cha Milundikwa wilaya ya Nkasi hivi karibu lengo ikiwa ni kubabiliana na tatizo la udumavu.

Wajumbe wa Kamati ya Lishe Mkoa wa Rukwa wakiwa wamenunua maboga lishe kwenye shamba la mkulima kijiji cha Milundikwa hivi karibu baada ya kukagua mradi huo wenye lengo la kufundisha umuhimu wa lishe bora kubaliana na udumavu.

Mwananfunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari Nkasi Fredrick Luwela akiwa ameshika sungura anaowafuga kama sehemu ya mradi wa kuboresha lishe bora na kujiongezea kipato chini ya mradi wa USAID/ Lishe Endelevu .

Mratibu wa Save the Children Rukwa Emanuel Magoyo (fulana nyeusi) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Lishe Mkoa ilipokagua shamba darasa la mboga mboga kijiji cha Milundikwa wilaya ya Nkasi chini ya mradi wa USAID/Lishe Endelevu mwishoni mwa wiki.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)

Post a Comment

0 Comments