Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YAPOKEA SHEHENA YA CHANJO YA UVIKO-19 AINA YA SINOPHARM.



*******************************

Na Richard Mrusha


Tanzania imepokea jumla ya chanjo (Dozi) 1,065,600 aina ya Sinopharm kutoka mpango wa COVAX Facility kwa ajili ya kuendelea kuwapatia wananchi chanjo dhidi ya UVIKO-19


Akiongea wakati wa mapokezi ya chanjo hizo Waziri wa Afya Maendeleo ya JamiiJinsia Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema chanjo hizo zimekuja na hivyo kuwapatia wananchi fursa ya kuchagua chanjo anayotaka kwani chanjo zote hizo ni salama zina ufanisi na ubora uliokubalika kisayansi na zimeonesha mafanikio makubwa katika kupunguza makali ya ugonjwa na kuepusha kifo.


“Ni dhahiri kuwa Serikali ya Tanzania imeonesha nia njema ya kuendelea kuwajali wananchi wake kama ambavyo imekuwa ikifanya siku zote kwenye sekta mbalimbali ikiwemo eneo la afya”.


Hata hivyo Dkt. Gwajima amesema Serikali inategemea kupokea chanjo za aina zingine katika wiki zijazo na itaendelea kutoa taarifa na utaratibu wa kila inapopokea ili wananchi wafahamu.


Kwa upande wa watanzania waliochanjwa Waziri huyo amesema hadi kufikia tarehe 7 Oktoba takwimu zinaonyesha wananchi waliochanjwa wamefikia 760,962 sawa na asilimia 74.4 kwa Tanzania Bara na 10,800 Zanzibar na kuongeza kuwa mwitikio ni mkubwa na chanjo za awamu ya kwanza zinatarajia kumalizika mwisho wa wiki ijayo.


Aidha, Dkt.Gwajima ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuendelea kusikiliza Serikali na Wataalamu wa afya na kujiepusha na habari zisizo rasmi”niwaombe tuwe makini na kusikiliza maelekezo tunayopewa na Wizara ya Afya hususani katika kujikinga na janga hili la kitaifa”.


Vilevile Dkt. Gwajima aliwasisitiza viongozi na watendaji wa ngazi zote kuendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuelimishwa na kuhimizwa kwenda kwenye vituo vya huduma za afya ili wakapate elimu kuhusu umuhimu wa chanjo.

Post a Comment

0 Comments