📌Wizara ya Maliasili na Utalii yajipanga kunadi Malikale kama fursa ujio wa AFCON
📌Maboresho maeneo ya Malikale kuvutia utalii wa ndani na nje ya nchi
📌Menejimenti ya Wizara na taasisi zake yahitimisha ziara maeneo ya Kaole, Ngome Kongwe na Caravan Serai
Na Neema Chalila Mbuja, Bagamoyo
IMEELEZWA kuwa ni muhimu kwa maeneo yenye Malikale kuenziwa na kutangazwa ili historia yake irithishwe kwa vizazi vijavyo.
Hayo yamesemwa leo Juni 28, 2026 mjini Bagamoyo na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Cristowaja Ntandu wakati wa kuhitimisha ziara ya Menejimenti ya wizara hiyo na taasisi zake waliokuwa wakitembelea maeneo ya Malikale na namna watakavyotumia fursa ya ujio wa Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON -2027) kunadi Malikale kuvutia watalii.
Ameyataja maeneo ya Malikale ambayo wajumbe wa Menejimenti wameyatembelea kuwa ni pamoja na mabaki ya Magofu ya Kaole, Ngome Kongwe eneo la Bagamoyo na eneo la njia ya msafara wa watumwa kutoka Kigoma Ujiji hadi Bagamoyo ambalo ndio lililokuwa Soko la Watumwa kwa Afrika Mashariki.
Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kamishna wa Kanda ya Mashariki wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) John Nyamuhanga amesema kuna haja ya kuhakikisha kuwa TANAPA inanadi historia ya nchi yetu ili kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni nane ifikapo mwaka 2030.
Amesema jamii inapaswa kurithishwa utalii wa Malikale na kuendelea kutoa mafunzo kwa jamii na wanafunzi ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu urithi wa Malikale uliopo.
Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii imehitimisha ziara yake ya kutembelea maeneo ya Malikale na kuafikiana kutumia vema uwepo wa Malikale kuitangaza Tanzania kwa kutumia fursa ya ujio wa AFCON na matukio mengine makubwa kutangaza utalii.













0 Comments