*****************************
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa OR TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu amezitaka asasi za kiraia (AZAKI) kufanya kazi kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa Ili kufikia lengo la pamoja la kuwahudumia wananchi.
Pia amezitaka kushirikiana na mabaraza ya Madiwani na kuyajengea uwezo wa kuandaa na kusimamia miradi ya kimaendeleo inayotekelezwa katika halmashauri hizo.
Waziri Ummy Mwalimu ameyabainisha hayo Jijini Dodoma wakati akifunga wiki za AZAKI iliyofanyika jijini Dodoma kwa wiki nzima kwa kuzikutanisha asasi mbalimbali hapa nchini ambapo amesema AZAKI ni chombo muhimu katika kuisaidia serikali kufikia malengo hasa ngazi za chini kwenye halmashauri.
“Wengi tumekuwa tukiangalia serikali kuu tu lakini huko kwenye halmashauri kuna fedha nyingi sana na usimamizi hauko vizuri hasa mchango wa madiwani lakini ninyi ni chombo muhimu sana na mpo kila mahala katika serikali za mitaa” amesema Mhe. Ummy.
Amesema katika maeneo mengi hakuna ushirikiano kati ya AZAKI na Mabaraza ya madiwani hivyo AZAKI ni muhimu zikashilikiana kutoa elimu pia amezitaka AZAKI kutoishia katika ngazi za chini bali washirikiane pia na Sekretarieti za mikoa katika miradi wanayoiendesha kwenye maeneo hayo.
Ameongeza kuwa “ tushirikiane pia kwenye kutoa elimu katika matumizi ya mapato na ubunifu wa miradi kwenye halmashauri mfano Jiji la Dar es saalam kwa robo ya mwaka wamekusanya takribani bilioni 17 fedha ni nyingi hivyo mnaweza kushiriki katika kushauri ni miradi ipi inaweza kuwanufaisha wananchi moja kwa moja” amesema.
Aidha amezitaka AZAKI kusaidia hasa katika ajira kwa vijana kwa kuwasaidia njia za kubuni miradi itakayowaingizia kipato hasa vijana wa maeneo ya vijijini ili kuondoa msongamano wa vijana wanahama kutoka vijijini kwenda mijini kutafuta maisha bali wawezeshwe njia za kupata kipato katika maeneo yao.
Amesema OR TAMISEMI na AZAKI ndio wanaofanya kazi moja kwa moja na watu wa chini ngazi za serikali za mitaa hivyo ni vyema wakashirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kutatua kero za wananchi katika maeneo mbalimbali pia akafungua milango kwa AZAKI kushauri mambo ambayo ni kikwazo kwa katika kutumiza wajibu wao.
Ameongeza kuwa “ pia ninyi AZAKI mtawanyike mikoa yote sio kujirundika katika Mikoa michache kwani kuna baadhi ya Mikoa hakuna AZAKI zinazofanya kazi au zipo kwa uchache sana hasa Mikoa ya kusini” amesema.
Kwa upande wake mshauri mwelekezi wa CSO bwana Justice Rutenge amesema ndani ya wiki ya AZAKI kulikwenda sambamba na uwasilishwaji wa maada na maonyesho ya kazi zinazofanywa na AZAKI ili wananchi wajue nini AZAKI inafanya na mchango wake katika maendeleo.
Amesema maada zilizowasilishwa katika wiki nzima ni mchango wa AZAKI katika mendeleo ya watu, mchango wa AZAKI katika kushiriki katika sera mbalimbali hapa nchini, kufanya kazi na wadau wengine katika sekta ya maendeleo, kuboresha ufanisi katika sekta na changamoto zinazoikabiri AZAKI.
0 Comments