Ticker

6/recent/ticker-posts

BIL.67 KUTOLEWA MIKOPO KWA VIKUNDI VYA WANAWAKE, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU


********************* 

Na Asila Twaha, OR - TAMISEMI 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa imepanga kutoa shilingi Bil. 67.6 kama Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu kwa mwaka wa fedha 2021/22. 

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo mapema leo Jijini Dodoma wakati akikabidhi hundi ya shilingi 1,039,050,000 kwa vikundi 48 vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. 

Akikabidhi hundi hiyo Waziri Ummy amesema ni jukumu la kila halmashauri kuhakikisha katika makusanyo yake ya ndani inatoa asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na walemavu. 

“Utoaji wa Mikopo hii ni kwa mujibu wa sheria na sio hisani hivyo kila Halmashauri ihakikishe inatoa mikopo hii kwenye vikundi vyenye sifa. 

“Nitoe rai kwa vikundi vyote vinavyokabidhiwa hundi ya mikopo leo hii, muende mkazitumie fedha za mikopo kwa malengo mliyoyakusudia, nikosa la Kisheria kutumia fedha hizi kinyume na mkataba kama umeomba kwa ajili ya biashara hakikisha unafanya biashara na si vinginevyo. 

“Fedha hizi zitumike kwenye shughuli zitakazoleta tija kwenye uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla” Waziri Ummy 

Pia Waziri Ummy amezitaka Halmashauri kutumia wataalam wake kutoa elimu kwa vikundi vinavyotaka kukopo jinsi ya kutumia fedha hizo kwa miradi yenye tija na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kurejesha haraka ili na wengine waweze kunufaika. 

Kwa upande wa mnufaika wa mikopo Bi.Gladius Jalee kutoka kikundi cha Jeshi Kubwa kilichopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza azma ya kuendelea kusimamia na upatikanaji wa fedha za mikopo kwa kueleza kuwa kundi lao mpaka sasa wamefikia hatua zuri ya ukopeshwaji kutokana na urejeshaji wao mzuri kuanzia kukopeshwa kutoka shilingi milioni moja mpaka sasa kufikia kukopeshwa shilingi milioni hamisini.

Post a Comment

0 Comments