Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA BUNGE YAKAGUA JENGO LA OSHA DODOMA


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Najma Murtaza Giga (Mb) (mwenye ushungi mwekundu) akiongoza kikao cha awali baina ya Kamati hiyo na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga na menejimenti ya OSHA muda mfupi kabla ya Kamati kukagua jengo jipya la Ofisi za OSHA jijini Dodoma.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda, akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa jengo jipya la Ofisi za OSHA Dodoma mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyolenga kukagua jengo hilo mara baada ya ujenzi kukamilika. Miongoni mwa majukumu ya Kamati hiyo ni kuzisimamia Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo OSHA.


Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, wakiwa wameambatana na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga walipokuwa wakitembelea maeneo tofauti ya jengo jipya la Ofisi za OSHA jijini Dodoma.


Jengo jipya la Ofisi za OSHA jijini Dodoma.

****************************

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imekagua jengo jipya la Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) lilipo Dodoma ambapo imeeleza kuridhishwa na ubora wa jengo husika.

Ukaguzi wa Jengo hilo ulitanguliwa na kikao kifupi ambapo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipokea taarifa ya ujenzi huo iliyowasilishwa na menejimenti ya OSHA ambapo kwa mujibu wa taarifa hiyo jengo hilo la ghorofa tano limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.8, kiwango ambacho ni chini ya makadirio ya awali ya bilioni 6.56 pamoja na kodi.

“Mradi huu wa jengo la Ofisi za OSHA Dodoma tumeutekeleza kwa muda wa miezi nane (8) kuanzia Agosti 22, 2020 hadi Aprili 21, 2021. Hivyo, kutokana na kutekeleza mradi huu kwa wakati pamoja na usimamizi mzuri uliofanywa na OSHA (mteja), Mkandarasi na Mshauri Mwelekezi, tumefanikiwa kuokoa zaidi ya milioni 650,” alieleza Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, katika taarifa ya ujenzi iliyowasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge.

Aidha, Bi. Mwenda aliongeza kuwa pamoja na kujenga jengo hilo kwa muda mfupi na kutumia gharama ndogo mradi huo umetekelezwa kwa kuzingatia Sheria na taratibu zote za ujenzi, viwango stahiki vya ubora, usalama pamoja na mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Wakizungumza mara baada ya kutembelea maeneo tofauti ya ofisi hiyo, wajumbe wa Kamati wamesema wamefarijika kuona kwamba mradi huo wa Ofisi za Taasisi ya serikali umetekelezwa kwa kuzingatia taratibu zote za ujenzi na viwango stahiki.

“Tumewahi kukagua majengo mengi sana kama Kamati lakini mimi niseme kwa mara yangu ya kwanza tumeweza kukagua jengo ambalo si tu wanakamati wameridhika nalo bali ni jengo ambalo Kamati yetu haijaona dosari. Hivyo, nimpongeze Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda na timu yake nzima ya menejimenti pamoja na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri (Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuzisimamia Taasisi mbalimbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo OSHA,” amesema Emmanuel Mwakasaka, Mjumbe Kamati ya Katiba na Sheria.

Mjumbe mwingine wa Kamati hiyo Bi. Ng’wasi Kamani amesema: “Moja ya majukumu ya Kamati yetu ni kusimamia Taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo OSHA, na leo tumepata bahati ya kutembelea jengo hili la OSHA ambapo tumeona limejengwa ndani na muda mfupi hivyo tulitarajiwa kuambiwa kwamba limejengwa kwa gharama kubwa lakini tumefurahi kusikia kwamba ujenzi umekamilika kwa bajeti ambayo ni chini ya makadirio ya awali lakini pia limejengwa kwa viwango stahiki.”

Kwa upande wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambayo OSHA ni Taasisi chini yake, kupitia Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Masuala ya Watu Wenye Ulemavu, imesema inajivunia mafanikio yaliyopatikana katika mradi huo ikiwemo ujenzi kufanyika katika viwango stahiki vya ubora pamoja na kutumia bajeti kidogo na hivyo kuokoa zaidi ya milioni 650.Jengo hilo limejengwa na Kampuni ya Ujenzi ya kizawa ya Estim Construction Co. Ltd chini ya Mshauri Mwelekezi Chuo Kikuu cha Ardhi na umetekelezwa kwa muda wa miezi nane tu ambapo katika kipindi hicho chote jumla ya ajira 682 wakiwemo watu wenye ulemavu zilitengenezwa na unatarajia kutengeneza ajira zaidi ya 1,500 mara baada ya jengo hilo kuanza kutumika.

Post a Comment

0 Comments