Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akiangalia eneo ambalo limejengwa vibanda vya wauza mihogo kando ya fukwe za Coco wakati wa ziara yake ya kutembelea fukwe hizo leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akizungumza na waandishi wa habari mara baada kutembelea fukwe za Coco leo Jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
****************************
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka ametembelea fukwe za Coco kujionea hali ya ujenzi wa vibanda vya biashara na kuangalia changamoto mbalimbali za kimazingira katika eneo hilo.
Amesema kuwa kuna athari mbalimbali za kimazingira ambazo zimeonekana katika ujenzi huo unaoendelea mahala hapo ambazo zimesababishwa na shughuli za kibinadamu zilizoko katika eneo hilo.
“Serikali inawajibika kulinda mazingira hususan kwenye maeneo ya fukwe ambazo kwa sasa tunaona zinaathirika sana na shughuli za kibinadamu, wote mmeona jinsi ambavyo kingo za bahari zinaliwa sababu ya changamoto ya mabadiliko ya tabianchi”
Akiongeza amesema kuwa Manispaa ya Kinondoni ndiyo wanasimamia eneo hilo na wanatakiwa kufuata utaratibu wa Athari za Tathmini ya Mazingira (TAM) kwani kuna athari za wazi kabisa amabazo zimeonekana ikiwepo suala la utupaji wa taka ngumu katika maeneo hayo ya fukwe. Je, mfumo unakuaje na mfumo wa maji taka katika eneo kama hilo lenye watu wengi ukoje? .
“Unapokuwa na idadi kubwa ya watu katika eneo hili lazima kuwa na sehemu za utupaji taka ngumu na mfumo wa maji taka yaani vyoo na usalama wao kwa ujumla watu wanapokuwa hapa unakuaje? wote mmeona mawe yenye ncha kali yako pembezoni mwa vibanda hivi vya biashara ”.
Amemaliza kwa kusema kuwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa miradi kama hiyo ni muhimu kwani nia na madhumuni ni kujiridhisha na mambo makubwa ya msingi ambayo yanaboresha afya na ustawi wa yule atakayepata huduma katika vibanda hivyo vya fukwe za coco.
“ Hatuangalii tu faida ya yule mjasiriamali wala faida ya yule anayewekeza kuuza bidhaa mbalimbali bali tunaangalia pia kwa mkazi anayekuja kufurahia hapa afya yake, usalama wake vikoje? Lakini pia ndani ya eneo hili la mita 60 ni haki ya kila mwananchi kukaa katika eneo hili na akawa salama, je ustawi wa mazingira ukoje na waliojenga hivi vibanda wanawajibika vipi kuhakikisha kuwa kuna usalama lakini pia mabadiliko ya tabia nchi yanadhibitiwa ili athari tunazoziona zisiendelee kuwepo yote hayo ni mambo ya Msingi tunayopaswa kuyafahamu kabla hatujaingia kuanza kuweka mradi wowote katika maeneo ya fukwe kama tunavyoona hapa coco" alimalizia Dkt. Gwamaka.
Baada ya kumaliza ziara hiyo Mkurugenzi Gwamaka aliahidi kuwasiliana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni pamoja na TAMISEMI na kuona ambavyo kwa pamoja wataweza kurekebisha na kuboresha yale ambayo walikua wamekusudiwa kuyafanya katika eneo hilo la fukwe za coco.
0 Comments