Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YADHAMIRIA KUMALIZA MIGOGORO YA ARDHI NCHINI


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Miembeni mtaa wa Nera kata ya Isamilo mkoani Mwanza wakati wa utatuzi wa migogoro ya ardhi mwishoni mwa wiki.Abuu Seif mtoto wa Mzee Seif ambaye ni msimamizi wa mirathi wa familia ya marehemu akionesha vielelezo vyake mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa utatuzi wa migogoro ya ardhi wilayani Nyamagana mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza Amina Makilagi akizungumza mbele ya wananchi waliojitokeza kusikiliza utatuzi wa migogoro ya ardhi wa familia ya marehemu Mzee Seif uliotatuliwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleoa ya Makazi Dkt Angeline Mabula mwishoni mwa wiki.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kuhusiana na mipaka ya eneo wanalostahili kumilikishwa familia ya marehemu Mzee Seif kutoka kwa Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Elia Kamihanda wakati wa utatuzi wa migogoro ya ardhi katika wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa mtaa wa Nera kata ya Isamilo mkoani Mwanza wakati wa utatuzi wa mgogoro wa ardhi wa familia ya marehemu Seif juu ya umilikishaji viwanja vilivyopo eneo la Miembeni mwishoni mwa wiki. (PICHA ZOTE NA YUSUPH LUDIMO MANISPAA YA ILEMELA).

*****************************

Na Mwandishi Wetu, MWANZA



Serikali ya awamu ya sita chini Rais Samia Suluhu Hasan imedhamiria kumaliza kero na migogoro ya ardhi nchini kwa kutatua iliyopo na kuweka mikakati ya kuzuia migogoro mipya ikiwemo utwaaji maeneo ya wananchi bila kulipa fidia



Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula mwishoni mwa jijini Mwanza wakati wa kutatua migogoro ya muda mrefu ya ardhi iliyopo wilaya ya Nyamagana ukiwemo mgogoro wa wananchi na Mwekezaji kampuni ya Pamba Engineering uliopo kata ya Mhandu.



Mgogoro mwingine ni baina ya Msimamizi wa Mirathi Ndugu Abuu mwana familia ya Marehemu Mzee Seif eneo la Miembeni mtaa wa Nera kata ya Isamilo kuhusu umilikishwaji eneo lao la urithi na ulipwaji fidia kwa wananchi wa mtaa wa Kisoko kata ya Luchelele kutokana na Serikali kutwaa eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa shule



Katika kutatua mgogoro kati ya wananchi na Mwekezaji Pamba Engineering Naibu Waziri Dkt Mabula ameelekeza wananchi kumilikishwa eneo linalolalamikiwa kati yao na Mwekezaji katika Kata ya Mhandu kufuatia wananchi hao kukidhi matakwa yote ya kisheria na kulipa gharama za umilikishaji huku Familia ya Marehemu Mzee Seif ikielekezwa kupatiwa viwanja Saba vilivyopatikana baada ya kupimwa eneo lao la asili alilolinunua marehemu baba yao miaka ya themanini kwa aliyeteuliwa kusimamia mirathi baada ya kujiridhisha



Kuhusu eneo la mtaa wa Kisoko kata ya Luchelele Mhe Dkt Mabula mbali na kuwataka wananchi wa mtaa huo kushirikisha viongozi waliopo katika maeneo yao kutatua kero mbalimbali za ardhi alimtaka Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Sekiete Yahaya kuhakikisha anawalipa fidia wananchi wote 20 waliotwaliwa maeneo yao na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule mapema kabla ya mwaka wa fedha 2021/2022 kuisha ambapo kiasi cha shilingi milioni 350 zinadaiwa na wananchi hao



‘’Nikuombe Mkurugenzi wananchi hawa wamekaa muda mrefu wakisubiri fidia wengine wameshindwa hata kuendeleza maeneo yao kwa sababu hawajalipwa fidia, naomba wananchi hawa walipwe wote kabla ya mwaka wa fedha wa sasa kuisha ‘’ Alisema Dkt Mabula



Kwa upande wake mkurugenzi wa jiji la Mwanza Sekiete Yahaya alisema kuwa, maeneo yanayotwaliwa kwa ajili ya taasisi za Serikali kama shule na huduma nyengine yatalipwa fidia kwa awamu mpaka deni lote litakapokwisha.



‘’Mhe Naibu Waziri naahidi kulipa fidia kwa awamu kuanzia kipindi hiki cha kati kati ya mwaka wa fedha 2021/2022 na kumaliza jumla ya milioni 150 kufikia mwishoni mwaka huu wa fedha’’ alisema Yahaya.



Naye Diwani wa kata ya Luchelele Vicent Lusana alifafanua kuwa wanafunzi wanaotoka eneo lake wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata elimu na kusisitiza kuwa ipo haja kwa Serikali kuharakisha ulipwaji wa fidia ili waanze ujenzi wa shule kwa lengo la kuwafanya wanafunzi wa eneo hilo kupata elimu katika umbali mfupi na kuwaepusha na changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni



Akihitimisha Kamishina wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Elia Kamihanda ametaka kuzingatiwa utengwaji maeneo kwa ajili ya shughuli za Umma katika zoezi la upimaji na upangaji wa mji huku akiwaasa wananchi kuhakikisha wanayalinda maeneo yote yanayotengwa kwa matumizi ya jamii ikiwemo malalo na maeneo ya wazi.

Post a Comment

0 Comments