Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA KUENDELEA KUTEKELEZA DIPLOMASIA YA UCHUMI KATIKA KUJILETEA MAENDELEO

Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi ili kuliletea Taifa maendeleo ya kiuchumi kupitia mahusiano na nchi mbalimbali, mashirika ya kikanda na kimataifa.

Balozi Rutagaruka ametoa wito huo hivi karibuni wakati wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu “Umuhimu wa Diplomasia ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa katika Kuwaletea Wananchi Maendeleo” uliofanyika kwa njia ya mtandao na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Wabunge, Mabalozi na Wanadiaspora.

Akizungumza kwenye Mdahalo huo akiwa jijini Dodoma, Balozi Rutagerua amesema kuwa, upo umuhimu mkubwa kwa Tanzania kuendelea kuimarisha mahusiano yake na nchi mbalimbali na mashirika ya kikanda na kimataifa ili inufaike kiuchumi kupitia fursa lukuki zilizopo nchini kama vivutio vya Utalii, fursa za Uwekezaji na Biashara pamoja na kuhakikisha wadau wote zikiwemo Taasisi za Umma na Binafsi, Mabalozi na Wananchi kwa ujumla wanashiriki kikamilifu katika kutekeleza mikakati mbalimbali iliyopo ili kufikia malengo kusudiwa kupitia Diplomasia ya Uchumi.

Ameongeza kusema kuwa, tayari mafanikio mengi yamepatikana kupitia utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ikiwemo kuimarika kwa Sekta za Uchumi ambapo tayari mikataba kadhaa ya manufaa kwa nchi imesainiwa ukiwemo ule wa Serikali ya Tanzania kuwa Mwenyeji wa Kampuni ya Mafuta Ghafi ya Afrika Mashariki (EACOP) itakayohusika na Ujenzi wa Mradi wa Bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga. Mafanikio mengine ni kuondolewa kwa vikwazo 46 kati ya 64 vya muda mrefu visivyo vya kiforodha kati ya Tanzania na Kenya. Vikwazo hivi vimeondolewa kufuatia ziara ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kenya mwezi Mei 2021.

Kadhalika amesema kuwa, Tanzania imeimarisha ushiriki wake katika masuala ya kikanda na kimataifa na kwamba mwezi Septemba 2021 Tanzania iliridhia Mkataba wa kuanzisha Eneo Huru la Biashara Barani Afrika na kwamba kuridhiwa kwa mkataba huu kumeongeza ushawishi wa Tanzania katika mtangamano wa Afrika na kuwa sehemu ya soko kubwa la Afrika lenye idadi ya watu wapatao bilioni 1.3. Aliainisha maeneo mengine ya mafanikio kuwa ni pamoja na kukua kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili na ufunguzi wa Balozi na Konseli Kuu ambapo hadi sasa Tanazania inazo Balozi 44 na Konseli Kuu 6.

Mbali na mafanikio hayo, Balozi Rutageruka amesema Serikali itaendelea kutekeleza kikamilifu mikakati iliyopo ya kutekeleza Diplomasia ya Uchumi ikiwa ni pamoja na kuvutia utalii, uwekezaji na biashara kwa kutumia maonesho na makongamano; kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa zinazopatikana katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa; kutafuta fursa za masomo na ufadhili; kubadilishana ujuzi katika nyanja mbalimbali kati ya Taasisi za Tanzania na Taasisi nyingine nje ya nchi na kutumia Balozi za Tanzania katika kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Korea ya Kusini, Mhe. Togolani Mavura ambaye wakati wa mdahalo huo alizungumzia umuhimu wa Diplomasia amesema ni muhimu kwa Tanzania kuendelea kuwekeza kwenye Diplomasia hususan kuimarisha ushirikiano na nchi zingine ili kuepusha migogoro ambayo husababisha nchi kupoteza mwelekeo na badala ya kuokoa fedha kwa ajili ya huduma muhimu za jamii kama maji, afya na umeme nchi zinajikuta zinawekeza kwenye masuala ya migogoro na vita ambayo hugharimu fedha nyingi.

Naye Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi, Mhe. Hoyce Temu amesema Tanzania chini ya Utawala wa Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kung’aa kimataifa na kwamba mashirika mbalimbali ya kimataifa yameonesha nia ya kuisaidia Tanzania kufikia malengo yake hususan kwenye agenda mbalimbali ikiwemo ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030.

Akichangia hoja wakati wa mdahalo huo, Bi. Loveness Mamuya ambaye ni Mtanzania anayeishi Marekani amesema Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nje (Diaspora) ipo tayari kushirikiana na Serikali katika kuchangia maendeleo ya nchi na kutoa rai kwa Serikali kuwashirikisha kikamilifu Diapora kwenye mipango mbalimbali ikiwemo kutafuta wawekezaji na wafanyabiashara wa uhakika kutoka kwenye maeneo waliyopo.

Mdahalo huo ambao umeandaliwa na Taasisi ya Watch Tanzania na kuwashirikisha wazungumzaji mbalimbali umeongozwa na Dkt. Hezron Makundi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Diplomasia ya Uchumi ni Mkakati wa nchi kushirikiana na mataifa mengine, mashirika au taasisi za kimataifa kujinufaisha kiuchumi kupitia biashara, uwekezaji, utalii na teknolojia.
Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka akizungumza wakati wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu "Umuhimu wa Diplomasia ya Uchumi na Ushirikiano wa Kimataifa katika kuwaletea Wananchi Maendeleo". Mdahalo huo ambao umeandaliwa na Taasisi ya Watch Tanzania umefanyika kwa njia ya mtandao hivi karibuni na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Mabalozi, Wanadiaspora, Wahadhiri na Wabunge.

Balozi Rutageruka akimsikiliza Mbunge wa Mtama, Mhe. Nape Nnauye alipokuwa anachangia hoja wakati wa mdahalo huo
Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi, Mhe. Hoyce Temu naye akizungumza wakati wa mdahalo wa kitaifa kuhusu Diplomasia ya Uchumi
Balozi wa Tanzania nchini Korea ya Kusini, Mhe. Togolani Mavura akizungumza wakati wa mdahalo huo
Mtanzania anayeishi Marekani Bi. Loveness Mamuya naye akichangia jambo wakati wa mdahalo kuhusu Diplomasia ya Uchumi huku Balozi Rutageruka akimsikiliza
Post a Comment

0 Comments