************************
Na WAMJW-DOM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima leo Desemba 15, 2021 amefanya mazungumzo na ugeni kutoka Shirika lisilo Lakiserikali la Medical Teams International ulioongozwa na Mkurugenzi Mkazi Dkt. George Mwita katika ofisi za Wizara Jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo Dkt. Gwajima amewapongeza kwa jitihada zinazoendelea kufanywa za kuwahudumia wananchi hususan katika kuboresha huduma za mama na mtoto, huduma ya Chakula cha kutosha kwa wagonjwa wenye maradhi sugu, kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na huduma za Rufaa.
Ameendelea kwa kupongeza huduma ya utoaji mafunzo kwa watoa huduma za afya inayofanywa na Shirika hilo ili kuwajengea uwezo zaidi katika utoaji huduma kwa jamii.
Aidha, katika mpango wake wa kutembelea huduma zinazotolewa na Mashirika yasiyo Yakiserikali kwenye maeneo wanayofanya kazi katika jamii, Dkt.Gwajima amewahakikishia Shirika hilo kuwatembelea ili kujionea na kujifunza namna Shirika hilo linavyotoa huduma kwa jamii.
Shirika la Medical Teams International linatekeleza miradi yake ya kuwahudumia wananchi katika Mkoa wa Kigoma kwenye kambi za Wakimbizi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo la Medical Teams International Dkt. George Mwita amemshukuru Waziri wa Afya kwa kuendelea kutoa fursa kwa Mashirika Yasiyoyakiserikali, huku akimhakikishia Dkt.Gwajima Shirika hilo litaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ili kuwasaidia wananchi katika jamii.
0 Comments