Ticker

6/recent/ticker-posts

2021 MWAKA ULIOBEBA MAJONZI, VILIO KWA WATANZANIA

Baadhi ya viongozi waliofariki dunia mwaka 2021

***

 Na JUMA ISSIHAKA

ZIKIWA zimesalia siku chache kuanza mwaka mpya wa 2022, huku 2021 ukibaki kuwa mwaka wa majonzi milele kutokana na kughubikwa na matukio ya vifo vya viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa nchi Hayati Dk. John Magufuli.

Pamoja na hali hiyo kutokea katika miaka mbalimbali, lakini kilichotokea 2021 litabaki kuwa pigo pekee na jipya kuwahi kushuhudiwa nchini.

Hayati Dk. John Magufuli (Machi 17, 2021)

Kifo cha Dk. Magufuli

Machi 17, 2021 ndiyo siku iliyovunja rekodi ya miaka yote tangu uhuru wa Tanzania Bara, baada ya Mkuu wa nchi kufariki akiwa nmadarakani.

Siku hiyo saa sita usiku, aliyekuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, alitoa taarifa kwa taifa kupitia vyombo vya habari kuhusu kifo cha Hayati Dk. Magufuli.

Ingawa taarifa hiyo rasmi ilitanguliwa na uvumi kadhaa, lakini haikutosha kuwaaminisha baadhi ya Watanzania hadi waliposhuhudiwa mwili wake ukiagwa maeneo mbalimbali.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa Rais wa Tanzania kufariki akiwa madarakani tangu nchi ilipopata uhuru wake.

Hayati Magufuli alifariki katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya mfumo wa umeme wa moyo yaliyomsumbua kwa miaka kadhaa.

Hayati Maalim seif Sharif Hamad (Februari 17, 2021)

Kifo cha Maalim Seif

Maalim Seif Sarif Hamad aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais nwa Zanzibar, alifariki Februari 2, 2021.

Kifo chake kilizua kilio kwa taifa kwani kilitokea miezi kadhaa tangu aapishwe kushika wadhifa wa Umakamu wa kwanza wa Rais Zanzibar baada ya maridhiano.

Alifariki jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi yaliyomsumbua kwa siku chache, huku akiacha historia ya kuwa mwanasiasa aliyekomaa katika maridhiano.

Maalim Seif ni miongoni mwa wanasiasa waliohusika wakati wa uasisi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)visiwani Zanzibar chini ya Chama cha Wananchi (CUF) na baadaye mwaka 2020 kufanya hivyo chini ya Chama cha ACT Wazalendo alichohamia kutoka CUF.

Kifo chake halikuwa pigo kwa wana ACT Wazalendo pekee bali hata serikali zote za muungano kwani katika moja ya hotuba zake alikuwa akisisitiza mshikamano na siasa za tija badala ya chuki.

Hayati Balozi John Kijazi (Februari 17, 2021)

Kifo cha Balozi Kijazi

Wakati kidonda cha msiba wa Maalim Seif hakijapona baadaye taifa lilitoneshwa na taarifa za kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi aliyefariki dunia Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Kifo cha Hayati Kijazi kilichukuliwa kuwa pigo zaidi kwa Hyati Dk. Magufuli kwani wengi walidai alikuwa rafiki wake wa karibu na Katibu wake hata ofisini.

Historia ya upole, unyenyekevu na uadilifu wa kiongozi huyo ndilo jambo lililowaliza wengi katika msiba wake.

Katika kutambua heshima yake ndani ya utumishi wa umma, Hayati Magufuli, aliupa mradi wa makutano ya Barabara Ubungo jina la kiongozi huyo (Kijazi Interchange) wakati wa uzinduzi wake Februari 24, 2021.

Hayati Mhandisi Patrick Mfugale (Juni 29, 2021)

Kifo cha Mfugale

29 Juni, 2021 taifa lilipokea taarifa nyingine ya kiongozi aliyekuwa na jina kubwa kutokana na umahiri wake katika shughuli za Uhandisi naye ni aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale.

Kifo cha kiongozi huyo kiliwastua wengi kwakuwa hakukuwa na taarifa za awali kuhusu kusumbuliwa na maradhi yoyote na kwamba alifariki jijini Dodoma eneo ambalo alikwenda siku moja kabla kwa ajili ya shughuli za kikazi.

Baadhi ya watumishi wa TANROADS waliwahi kueleza kwamba Hayati Mfugale aliwaaga kwa furaha akienda jijini Dodoma lakini ulirejea mwili wake akiwa ameshafariki.

Walimtaja kuwa miongoni mwa viongozi waliofanikiwa kuiongoza taasisi hiyo, hivyo kuwafanya wafanyakazi wote kuishi kama familia moja, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Fedha, Hijja Malamla na Mkurugenzi wa Miradi TANROADS, Mhandisi Crispianus Ako.

Hayati Anna Mghwira (Julai 22, 2021)

Kifo cha Anna Mghwira

Julai 22, 2021 Tanzania ilipokea taarifa ya msiba mwingine wa mwanasiasa mkomavu na mwanamke aliyekuwa na rekodi ya pekee kuwania Urais kwa tiketi ya ACT Wazalendo mwaka 2015, Anna Mghwira.

Hayati Mama Mghwira alifariki siku chache baada ya kustaafu kazi ya Ukuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, wadhifa ambao aliteuliwa na Hayati Dk. Magufuli, wakati huo akiwa mwanachama wa ACT-Wazalendo kabla ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pamoja na kushindwa urais katika uchaguzi wa mwaka 2015, lakini alivunja rekodi ya kuwa mwanamke pekee aliyewania wadhifa huo nchini kupitia tiketi ya ACT-Wazalendo.

Alishindwa nafasi ya Urais kwa kupata kura 323,112 sawa na asilimia 2.22 ya kura zote 14,574,957 zilizopigwa.

Hayati Mhandisi Elias Kwandikwa (Agosti 2, 2021)

Kifo cha Kwandikwa

Agosti 2, 2021 pigo jingine lililikumba taifa la Tanzania baada ya kutangazwa kifo cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhandisi Elias Kwandikwa.

Kifo cha kiongozi huyo kilitokea jijini Dodoma huku viongozi mbalimbali waliowahi kufanya naye kazi wakimuelezea kwa sifa ya upole na unyenyekevu, alieleza aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ambaye walifanya kazi katika wizara moja akiwa Naibu wake.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Jina lake Lihimidiwe!Post a Comment

0 Comments