Ticker

6/recent/ticker-posts

MZEE KIMITI AWATAKA WANA RUKWA KUIUNGA MKONO SERIKALI

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (katikati ) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Jukwaa la Maendeleo Rukwa jana mjini Sumbawanga.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Sumbawanga Mjini Aeshi Hilary jana kwenye mkutano Mkuu wa Jukwaa la Maendeleo Rukwa (JUMARU). Mzee Paul Kimiti (81) ambaye ni Waziri Mstaafu akizungumza kwenye mkutano Mkuu wa Jukwaa la Maendeleo Rukwa jana mjini Sumbawanga ambapo amewaasa wananchi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wa serikali kusukuma maendeleo. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti. Mwenyekiti wa JUMARU Bi. Helena Khamsini akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Jukwaa la Maendeleo Rukwa jana ambapo alisema lengo la jukwaa hilo ni kuhamasisha na kuchangia jitihada za kuleta maendeleo ndani ya mkoa wa Rukwa.

***************************

Waziri Mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyehudumu tangu Awamu ya kwanza hadi ya tatu Paul Kimiti ametoa wito wa wananchi wa mkoa wa Rukwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali ili kusukuma agenda ya maendeleo Rukwa.

Mzee Paul Kimiti (81) ambaye amewahi kuhudumu kama Waziri, Mbunge na Mkuu wa Mkoa kwa nyakati tofauti ametoa rai hiyo (27.12.2021) mjini Sumbawanga wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Jukwaa la Maendeleo Mkoa wa Rukwa (JUMARU).

“Tusipo isaidia serikali tutakaoumia ni sisi wananchi. Tuwasaidie viongozi wetu Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa wilaya watekeleze majukumu yao kwa ufanisi ili Rukwa ipige hatua za kimaendeleo” alisema Mzee Kimiti.

Aliongeza kusema JUMARU haipaswi kutumika kama jukwaa la kisiasa bali lengo lake liwe kuibua hoja na agenda za kuisaidia serikali kupanga mipango ya kiuchumi kwa maslahi ya wana Rukwa.

“Kaeni kama pete na kidole. JUMARU na serikali wafanye kazi kwa pamoja. Msigombane kwenye makundi ya whatsapp (mitandao ya kijamii) hayasaidii kuijenga Rukwa kimaendeleo” alisisitiza Mzee Kimiti.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alieleza masuala manne muhimu kwa Jukwaa hilo kwanza , JUMARU kuibua hamasa ya maendeleo kwa kujenga ushawishi kwa wadau ili wachangie ukuaji uchumi wa Rukwa.

Jambo la pili, JUMARU iwatumie wazee maarufu na vijana wenye mawazo chanya kuweka mipango endelevu ya kufanya mkoa wa Rukwa upige kasi ikiwemo miradi ya maendeleo na tatu, jukwaa hilo litumike kupata agenda za kuiwezesha serikali kuchukua hatua za kusimamia maendeleo ya wananchi.

Mkirikiti alitaja jambo la nne kwa JUMARU kuwa ni kuhamasisha sekta ya michezo ili ichangie zaidi katika kuzalisha ajira hususan kwa vijana na kufanya mkoa wa Rukwa utambulike na kuchangia zaidi kwenye pato la taifa huku akitolea mfano uwepo wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania Prison na manufaa ya kiuchumi yanayopatikana Sumbawanga.

“Rukwa bado tupo nyuma kimaendeleo hivyo ni jukumu la JUMARU kushauri serikali namna gani ya kufanya kilimo kichangie zaidi kwenye uchumi na sekta zingine ikiwemo ushirika ambao una nafasi kubwa kuondoa unyonyaji kwa wakulima wadogo” alisema Mkirikiti.

Naye Mwenyekiti wa JUMARU Helena Khamsini alisema dira ya jukwaa hilo ni kuwa na Rukwa yenye maendeleo endelevu katika nyanja zote hususan elimu, afya, mazingira, uchumi na utamaduni.

Mkutano huo Maalum umehudhuriwa na Wazee maarufu, viongozi wa kimila, viongozi wastaafu wa serikali, vijana, wawakilishi wa akina mama na wasanii.

Post a Comment

0 Comments