Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema mfumo wa “Ongea na Waziri” ni daraja muhimu kati ya serikali na wananchi unaolenga kusikiliza moja kwa moja maoni, kero na mapendekezo ya wananchi kuhusu huduma za afya.
Amesema mfumo huo, uliozinduliwa rasmi Januari 26, 2026, unalenga kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya na kuhakikisha maamuzi ya serikali yanaendana na mahitaji halisi ya wananchi.
Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo Machi 13, 2026 wakati wa ziara yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jijini Dar es Salaam, ambapo pia alishiriki katika tukio la “Ongea na Waziri” lililowakutanisha watumishi wa afya na wananchi kwa lengo la kusikiliza changamoto na kupokea maoni kuhusu utoaji wa huduma za afya.
Amesema kuanzishwa kwa mfumo huo kunaonesha dhamira ya serikali ya kuweka kipaumbele katika kusikiliza wananchi kama msingi wa kuboresha huduma na kuimarisha uwajibikaji katika sekta ya afya.
Aidha, Waziri Mchengerwa amesema serikali ipo mbioni kuandaa mwongozo utakaotumika katika hospitali zote za serikali ili kukabiliana na malalamiko ya wananchi kuhusu gharama kubwa za matibabu na upatikanaji wa dawa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amesema mfumo wa kidijitali wa “Ongea na Waziri” ulioanzishwa na Waziri Mchengerwa unalenga kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta ya afya.
Dkt. Shekalaghe amesema kupitia mfumo huo wananchi wanapata nafasi ya kuwasilisha changamoto na maoni yao moja kwa moja kwa Waziri, jambo linalosaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa haraka na kuimarisha utoaji wa huduma za afya.
Ameongeza kuwa wizara itafanya majumuisho ya maswali yaliyoulizwa katika mwezi uliopita ili kutathmini ni maswali mangapi yamepatiwa majibu pamoja na hatua zilizochukuliwa katika kuyatatua.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Mwananyamala, Evancy Asenga, amemshukuru Waziri Mchengerwa kwa ziara yake hospitalini hapo na kuahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa ili kuboresha huduma, hususan katika eneo la mapokezi ya wananchi.
Pia ameomba serikali kufanikisha ujenzi wa jengo kubwa la ghorofa katika hospitali hiyo ili kurahisisha utoaji wa huduma.
Asenga amesema hospitali hiyo imefanikiwa kufanya mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dkt. Mercy Maya, amesema hospitali hiyo inaendelea kuimarisha na kupanua huduma za kibingwa kwa kuboresha miundombinu na kuongeza vifaa tiba ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.





0 Comments