Ticker

6/recent/ticker-posts

PROF. MBARAWA AVUNJA BODI YA TPA NA MSCL


**********************

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amevunja Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), na Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), kwa sababu ya uzembe na usimamizi mbovu wa miradi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa maboresho ya Gati namba 0 hadi 7 na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa miundombinu ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Pili (km 20.3) uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

"Leo tarehe 04/12/2021 kwa Mamlaka niliyonayo nimetengua Bodi za Wakurugenzi wa TPA na MSCL kutokana na kutokuwajibika ipasavyo katika kutoa ushauri na wakati wa ubadhirifu na ukiukwaji wa vipengele katika mikataba ya miradi walikuwepo", amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesema kuwa uamuzi huo umetokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoridhishwa na utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam hasa katika usimamizi wa gati hizo zilizoboreshwa kutokuwa mzuri na kusababisha kuwepo kwa marekebisho ya baadhi ya gati ili viendane na viwango vinavyostahili kulingana na mkataba.

Prof. Mbarawa ameeleza pia kumeripotiwa matukio ya wizi katika mifumo ya bandari ambapo mkandarasi aliyefunga hiyo mifumo hakuitekeleza ipasavyo na kuacha mianya ya wizi ukaendelea.

Kwa upande wa Kampuni za Huduma za Meli Tanzania (MSCL), Prof. Mbarawa amebainisha kumekuwa na mapungufu kwa mkandarasi aliyeshinda kazi za ujenzi wa meli nne zinazotarajiwa kujengwa katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Bahari ya Hindi.

"Baada ya utiaji saini mikataba minne tarehe 15 Juni, 2021 Serikali ilitilia shaka uwezo wa mkandarasi na kuamua kufanya ufuatiliaji wa uwezo wa mkandarasi huyo aliyeshinda zabuni na kubaini kuwa hana uwezo wa kutengeneza meli na hakuwa na ofisi”, amefafanua Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa ametoa rai kwa watendaji wote waliopo chini ya Wizara yake kuwa waadilifu na kusimamia kwa karibu miradi yote inayoendelea kutekelezwa.

"Naomba nichukue fursa hii kuwataka watendaji wote kuwa waadilifu, wazalendo, tuumwe na nchi hii katika miradi ya kiamaendeleo", amesisitiza Prof. Mbarawa.

Bodi ya Wakurugenzi ya TPA ilikuwa na jumla ya wakurugenzi saba (7) ikiongozwa na Mwenyekiti Prof. Ignas Rubalatuka na Bodi ya MSCL ina wakurugenzi watano (5) ikiongozwa na Mwenyekiti Prof. Zacharia Mganilwa.

Post a Comment

0 Comments