Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AIPONGEZA TARURA KWA USIMAMIZI WA UJENZI WA BARABARA ZA MJI WA SERIKALI MTUMBA



********************

Na. Erick Mwanakulya, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), amepongeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Serikalii Mtumba zenye urefu wa Km 51.2.

Mhe. Majaliwa ametoa pongezi hizo leo tarehe 02 Desemba, 2021 alipokuwa akikagua ujenzi wa miradi ya maendeleo iliyopo katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa awamu ya pili ya ujenzi wa ofisi za Wizara katika mji huo.

“Nawapongeza TARURA pamoja na OR-TAMISEMI kwa usimamizi mzuri wa barabara, kimsingi viwango vya ujenzi vinaonekana na vinaridhisha, barabara ni nzuri nimesikia kazi ambazo zimefanyika na ambazo zitakamilika katika kipindi ambacho mmekubaliana kwenye mkataba”, amesema Mhe. Majaliwa.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor H. Seff amesema ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali Mtumba unahusisha ujenzi wa barabara za njia 4 Km 22.4 na ujenzi wa barabara za njia 2 Km 28.8 ambazo ni barabara zenye jumla ya urefu wa km 51.2.

Mhandisi Seff amefafanua kuwa barabara hizo zimejengwa kwa kiwango cha “super pave” huku akiongeza kuwa kazi nyingine zinazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja 10 na makalavati 106, mifereji ya maji ya mvua km 78.24 na huduma zote zilizoainishwa kwenye usanifu.

Kuhusu mkandarasi anayetekeleza mradi huo, Mhandisi Seff amesema kuwa mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Ltd (CHICO), ambapo umefikia asilimia 88 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 31/12/2021.

Aidha, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim majaliwa mbali na ukaguzi wa barabara za Mji wa Serikali Mtumba pia ameweka jiwe la msingi katika jengo la kituo cha polisi Mtumba Daraja A, amefanya ukaguzi wa jengo la Kitega uchumi la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, pamoja na uzinduzi wa ujenzi wa ofisi za wizara zinazojengwa kwa awamu ya pili katika Mji wa Serikali Mtumba.

Post a Comment

0 Comments