Ticker

6/recent/ticker-posts

MABALOZI WA KODI WAWAASA WANANCHI KUACHA BIASHARA YA MAGENDO

Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Soda cha Anjari kilichopo Mkoani Tanga Bw. Safari Mngazija akiwaonyesha Mabalozi wa Kodi jinsi kiwanda hicho kinavyofanya kazi wakati wa ziara yao ya kikazi katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga iliyolenga kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na wakati.

Mabalozi wa Kodi wakiwa katika eneo la Bandari ya Tanga wakati wa ziara yao ya kikazi katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga iliyolenga kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na wakati. (PICHA ZOTE NA TRA).

***********************

Na Mwandishi wetu
Tanga

Wito umetolewa kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuacha biashara ya magendo kwani vitendo hivyo vinaikosesha Serikali mapato yake stahiki kutokana na wahusika wa biashara hizo kukwepa kulipa kodi.

Wito huo umetolewa na Mabalozi wa Kodi ambao ni Mhe. Zulfa Omar, ambae ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba, Mhe. Subira Mgalu Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani na Bw. Edo Kumwembe ambaye ni Mwandishi wa Habari wakati wa ziara yao ya kikazi katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga iliyolenga kuhamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari.

“Katika ziara yetu, tumepita katika mipaka mingi na kila mipaka tuliyopita tumekuta kuna changamoto ya magendo, wananchi wanapitisha bidhaa kwenye njia zisizo rasmi na ukiwahoji, baadhi yao wanakuambia wao wamezaliwa, wanasoma na wanakula kwa kufanya biashara hiyo.

Niwaombe sana wananchi, tusiishi kwa mazoea, tuache kabisa biashara hii kwasababu sote tunafahamu kwamba, kulipa kodi ndio njia inayotuwezesha kujenga Tanzania yetu na mimi kama balozi nitaendelea kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuacha biashara hii ya magendo,” alisema Balozi Zulfa.

Naye, Balozi Edo Kumwembe alieleza kuwa, sababu kuu ya kuwahamasisha wananchi kuacha biashara ya magendo ni kukosekana kwa uhakika wa ubora wa bidhaa zinazopitishwa katika njia zisizo rasmi na hivyo zinaweza kuhatarisha afya ya wananchi.

“Dhumuni la kuzuia biashara ya magendo kwanza ni kutukosesha mapato lakini vilevile hatuna uhakika na ubora wa bidhaa zenyewe kiasi kwamba zinaweza kuleta athari kwenye afya za walaji,” alisema Balozi Kumwembe.

Kwa upande wake Balozi Subira Mgalu amewaomba wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na kuacha kupitisha bidhaa kwenye njia za panya ambapo wakikamatwa bidhaa zao zote na vyombo vya usafiri vilivyotumika kusafirishia bidhaa hizo hutaifishwa ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungwa jela.

Ziara ya mabalozi hao katika Mikoa ya Kasikazini imemalizika leo ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo amesema kuwa, TRA itaendelea kutoa ushirikiano kwa mabalozi hao ili kuhakikisha wanafanya kazi yao ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kulipa kodi kwa hiari na wakati.

Mabalozi hao wa kodi walioteuliwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wakati akihitimisha mjadala wa Bunge la Bajeti mwezi Juni, 2021, wamepata fursa ya kutembelea mipaka ya Namanga, Holili na Tarakea iliyopo katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Post a Comment

0 Comments