Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS DKT. MAPANGO ATEMBELEA HIFADHI YA GOMBE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe iliopo mkoani Kigoma kwaajili kufanya kutembela na kufanya utalii katika hifadhi hiyo. Januari 28,2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akipokea maelezo ya historia na mwenendo wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe kutoka kwa Mkuu wa Hifadhi hiyo Yustin Njamasi wakati Makamu wa Rais alipotembelea hifadhi ya hiyo tarehe 28 Januari 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akipokea maelezo kutoka kwa mkurugenzi wa utafiti wa taasisi ya Jane Goodall Dkt. Deus Mjungu juu ya ufuatiliaji wa vizazi vya sokwe unaofanywa katika maabara ya utafiti iliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe. Januari 28,2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akipanda mti wa chakula cha Sokwe katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe alipoitembelea hifadhi hiyo tarehe 28 Januari 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitembea katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe kujionea vivutio mbalimbali. Januari 28,2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa na mkurugenzi wa utafiti wa taasisi ya Jane Goodall Dkt. Deus Mjungu katika nyumba aliokuwa akiishi Dkt. Jane Goodall wakati akifanya tafiti mbalimbali za Sokwe waliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango pamoja na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma wakati Makamu wa Rais alipotembelea hifadhi hiyo tarehe 28 januari 2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakiwa katika Picha ya Pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma na Mkuu wa Hifadhi ya Gombe wakati wakiondoka mara baada ya kumaliza kutembelea hifadhi hiyo tarehe 28 Januari 2022.

***********************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 28 Januari 2022 ametembelea hifadhi ya Taifa ya Gombe iliopo mkoani Kigoma. Makamu wa Rais amejionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika hifadhi hiyo maarufu kwa upatikanaji wa Sokwe, pamoja na miti ya asili iliochanganyika kutoka Afrika ya kati na Afrika Afrika Mashariki.


Akiwa katika hifadhi hiyo Makamu wa Rais ametembelea maabara ya utafiti inayotumika kutafiti uzao wa sokwe na kutambua kizazi halisi cha sokwe hao. Aidha Makamu wa Rais ametembelea nyumba alioishi mtafiti wa kwanza wa kimataifa wa Sokwe Dkt. Jane goodall alipokuwa hifadhini hapo.


Mkurugenzi wa utafiti wa taasisi ya Jane Goodall Dkt. Deus Kijungu pamoja na wahifadhi wa hifadhi hiyo wamemueleza Makamu wa Rais changamoto ya uharibifu wa mazingira inayofanywa na baadhi ya wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo pamoja na wale wanaotoka mataifa jirani. Aidha wamesema sokwe hao wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya mlipuko yanayopelekea vifo vyao.


Akizungumza baada ya kutembelea hifadhi hiyo, Makamu wa Rais amewapongeza wahifadhi na watafiti waliopo katika hifadhi hiyo kwa jitihada kubwa wanazofanya kulinda sokwe waliopo hifadhini humo. Makamu wa Rais amewahimiza watafiti kujielekeza katika tafiti za kukabiliana na magonjwa yanayosumbua sokwe hifadhini hapo ili kupunguza hatari ya kupotea kwa sokwe hao wakati ujao.


Aidha Makamu wa Rais ameutaka uongozi wa mkoa wa Kigoma kutoa elimu pamoja na kupambana na vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyofanywa na wananchi waliopo maeneo jirani na hifadhi hiyo. Amesema wakati wote ni muhimu kuzingatia taratibu za kuingia na kutoka katika hifadhi hiyo ili kupunguza hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoweza kuwapata sokwe hifadhini.


Makamu wa Rais amewataka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) kuhamasisha utalii wa ndani utakaochochea ukuaji wa mapato pamoja na ulinzi wa hifadhi zilizopo nchini. Amesema ni muhimu kwa viongozi wa mikoa na wilaya kuwa mstari wa mbele na wa mfano katika kutembelea vivutio vya utalii ili kujua changamoto zilizopo na kuzitatua.


Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameagiza kuongezwa kasi ya upandaji miti ya chakula cha Sokwe katika hifadhi ya Gombe ili kuwarahisishia sokwe hao upatikanaji wa chakula. Amesema sambamba na miti hiyo lakini pia ni muhimu kupanda miti itakayozuia mmomonyoko wa udongo katika eneo hilo.


Makamu wa Rais amesema serikali inaendelea na jitihada za kukuza sekta ya utalii hapa nchini ikiwemo kutengeneza barabara itakayotumika kufika katika hifadhi hiyo na kuondokana na usafiri wa aina moja pekee wa njia ya maji kufika hifadhini hapo.

Post a Comment

0 Comments