Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS DKT.MPANGO ATEMBELEA BONDE LA MUZAKWE


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitoa maelekezo ya uhifadhi wa Mazingira katika Bonde la Mzakwe na maeneo mengine kwa viongozi wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya kutembelea na kukagua miti iliopandwa katika bonde hilo. Januari 5,2021.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitembelea na kukagua zoezi la upandaji miti na uhifadhi katika Bonde la Mzakwe lililopo mkoani Dodoma. Januari 5,2021


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akitoa maelekezo kwa meneja msaidizi maendeleo ya misitu kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS kanda ya kati) Bi. Patricia Manonga wakati alipofika kukagua upandaji miti na uhifadhi wa bonde la mzakwe Mkoani Dodoma.

PICHA – OFISI YA MAKAMU WA RAIS

***********************

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 05 Januari 2022 ametembelea na kukagua zoezi la upandaji miti na uhifadhi wa bonde la Mzakwe lililopo mkoani Dodoma.



Akikagua uhifadhi wa bonde hilo ambalo pia ni chanzo cha maji , Makamu wa Rais ameoneshwa kutoridhishwa na usimamizi na ufuatiliaji wa uhifadhi wa bonde la mzakwe uliopelekea kupotea kwa miti iliopandwa hapo awali kutokana na moto uliotokea novemba mwaka 2021 pamoja na baadhi ya miti mingine kushindwa kustawi. Makamu wa Rais amewataka viongozi wa TFS pamoja na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla kushirikisha jamii katika uhifadhi ili wananchi watambue umuhimu wa miti hiyo pindi inapopandwa katika maeneo yao.



Aidha Makamu wa Rais amewataka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori) kuwa na uhakika wa aina ya miti inayoweza kustawi katika bonde hilo ikiwemo miti ya asili. Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuainisha miti inayopandwa pamoja na malengo yake ili kuepusha miti inayoweza kuwa chanzo cha kupoteza maji na ile itakayoshindwa kustawi katika eneo hilo.



Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewaasa viongozi wa mkoa wa Dodoma kuangilia sheria ndogondogo zitakazowezesha wananchi kufanya upandaji wa miti hasa katika maeneo ya ujenzi wa majengo ya makazi na yale ya biashara ili kutunza mazingira na kuongeza uwezekano wa upatikanaji mvua kwa wingi mkoani Dodoma.



Makamu wa Rais amesema utekelezaji wa kampeni ya kuifanya Tanzania kuwa ya kijani ni wajibu wa kila mtanzania na kuwaagiza wakuu wa mikoa, Wilaya , Wakurugenzi , na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, watendaji wa kata na vijiji kuongoza zoezi la upandaji miti na kuisimamia kikamilifu.



Kwa upande wake katibu tawala wa mkoa wa Dodoma Dkt. Fatuma Mganga akizungumza kwa niaba ya viongozi walioshiriki ziara hiyo amesema maelekezo yote yaliotolewa na Makamu wa Rais yatafanyiwa kazi kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha zoezi la kuifanya Dodoma kuwa ya kijani. Amesema tayari mkoa wa Dodoma umeandaa miche milioni mbili na tayari maandalizi yamefanyika katika taasisi zote zilizopo mkoani Dodoma zitakazokabidhiwa miche hiyo katika kutekeleza zoezi la kuifanya Dodoma iwe ya kijani.

Post a Comment

0 Comments