Arusha
Tume ya Madini imeanza rasmi kutumia Mfumo Jumuishi wa Kodi za Ndani (IDRAS) unaolenga kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi wa utendaji na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali katika sekta ya madini.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi cha wahasibu na wachumi wa Tume ya Madini kilichomalizika leo mkoani Arusha kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Nsajigwa Kabigi, amesema mfumo huo utawawezesha wateja kujihudumia saa 24 popote walipo na kuharakisha utoaji wa huduma.
Amesema matumizi ya IDRAS yataongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato huku yakirahisisha huduma kwa wananchi na wadau wa sekta ya madini.
“Tunatarajia mfumo huu kuongeza mapato ya Serikali na kuwapa wateja huduma kwa haraka na urahisi zaidi,” amesema Kabigi.
Kabigi pia amewataka wahasibu na wachumi kuwa makini katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa kuzingatia usalama wa taarifa na nyaraka zinazotumika kupitia mfumo huo.
Aidha, amesema Serikali imeiwekea Tume ya Madini lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.4 katika mwaka wa fedha 2026/2027 baada ya kufikia makusanyo ya shilingi trilioni 1.2 hadi Mei 18 mwaka huu kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Tume ya Madini, CPA Idfonce Masoud, amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wahasibu na wachumi kuhusu matumizi ya mfumo mpya pamoja na utekelezaji wa sheria za kodi.
Amesema washiriki wamepata uelewa kuhusu ukokotoaji wa kodi ya zuio, PAYE na namna ya kuwasilisha taarifa za kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Masoud ameongeza kuwa wahasibu wanapaswa kuendana na viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu ili kuhakikisha taasisi zinaandaa taarifa za fedha kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.







0 Comments