Ticker

6/recent/ticker-posts

MASOKO ZAIDI YA PARACHICHI YA TANZANIA YAZIDI KUFUNGUKA ULAYA, NAIBU WAZIRI MAVUNDE AWAPA TARI JUKUMU MAHSUSI


*****************

Soko la parachichi ya Tanzania katika nchi za Jumuiya ya Ulaya limezidi kufunguka kufuatila Kampuni ya Kilimo ya GIBRI ya Iringa kuingia mkataba wa makubaliano ya ununuzi wa parachichi na makampuni makubwa ya nchini Hispania.

Maelezo hayo yametolewa jana wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mavunde katika Pack House na kitalu cha miche ya parachichi vilivyopo eneo la Ipogolo, Iringa Manispaa ambavyo vyote vinasimamiwa na kampuni ya kilimo ya GIBRI.

Akitoa maelezo hayo, Mkurungenzi Mkuu wa Kampuni ya GIBRI Bi. Khadija Jabir amemueleza Naibu Waziri Mavunde kwamba Kampuni yake imeingia makubaliano na wanunuzi wa parachichi kutoka nchini Hispania ambayo imepelekea pia wao kuingia makubaliano na AMCOS za wakulima wa parachichi zipatazo 9 kwa ajili ya manunuzi ya parachichi hizo mpango ambao unategemewa kuwanufaisha zaidi ya wakulima 3000.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mavunde alipata fursa pia kuwatembelea mashambani mwao wakulima wa parachichi wa Wilaya ya Kilolo, Iringa yanayomilikiwa na Bw. Chesco Mdeka na Bw. Steve Lawrie yaliyopo katika vijiji vya Lulanzi na Lukani mtawalia ili kujionea hali ya uzalishaji wa mapachichi na kuagiza Taasisi ya Utafiti ya Kilimo Nchini(TARI) kuharakisha uanzishwaji wa kitalu cha miche bora ya parachichi wilayani Kilolo ili kuongeza wigo wa uzalishaji wa zao hilo ambalo hivi sasa soko lake limekuwa kubwa nje ya nchi.

“Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta masoko zaidi ya parachichi na kwasasa tumeshapata vibali vya kupeleka parachichi katika Nchi India na Afrika ya Kusini,tukisubiri ukamilishwaji wa taratibu za matakwa ya usafirishaji wa mazao kwa Nchi za China na Marekani.

Soko hili litakuwa kubwa sana hivyo ni vyema tujipange mapema kuanzia katika ubora wa miche ya parachichi sambamba na kuongeza maeneo zaidi ya uzalishaji wa parachichi.

Nitoe rai kwa Watanzania kuchangamkia fursa hii ya soko la zao la parachichi kwa kushiriki kwenye kilimo hichi, na sisi kama Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan tutahakikisha tunatoa huduma zote muhimu za kitaalamu ili kumuwezesha mkulima kufikia malengo yake” Alisema Mh. Mavunde

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mbunge wa Kilolo *Mh Justine Nyamoga* ameiomba Serikali kusaidia kupatikana kwa miche ya parachichi yenye ubora na kwa gharama ambayo mkulima ataimudu ili kuchochea kasi ya ulimaji wa zao hilo wilayani Kilolo ambapo zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wa eneo hilo wanajishughulisha na shughuli za kilimo..

Post a Comment

0 Comments