Ticker

6/recent/ticker-posts

MHANDISI KASEKENYA AWATAKA TANROADS KUONGEZA KASI UJENZI NJIA NANE


Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam, Eng. Harun Senkuku akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya (kulia), alipokagua ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (njia nane), jijini Dar es Salaam.


Mhandisi Mwanaisha Rajabu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya (kushoto) alipokagua ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (njia nane), jijini Dar es Salaam.


Muonekano wa daraja la waenda kwa miguu lililopo Stendi Kuu ya Mabasi ya Mikoani (Magufuli Terminal) katika barabara ya Morogoro sehemu ya Mbezi, jijini Dar es Salaam.


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya akiwa na wataalam wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (njia nane), jijini Dar es Salaam.


Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam, Eng. Harun Senkuku (kulia) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya (katikati) alipokagua ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (njia nane), jijini Dar es Salaam, kulia ni Eng. Mwanaisha Rajabu akifuatilia.

**************************

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya ameuagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha maboresho yanayofanywa katika ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (njia nane), yanakamilika ifikapo Juni mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya Ujenzi huo, Eng. Kasekenya amewataka wataalam wanaosimamia maboresho ya barabara hiyo waendelee na zoezi la utoaji elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara hiyo ili kupunguza ajali.

“…TANROADS shirikianeni na askari wa usalama barabarani kutoa elimu ya namna bora ya kutumia vivuko vya juu na chini ya barabara pindi ujenzi wake unapokamilika na kuhakikisha barabara zinakuwa safi wakati wote,” amesema Naibu Waziri Eng. Kasekenya.

Amewaonya wote wanaoharibu alama za barabara na kutupa taka ngumu kuacha mara moja uharibifu huo na kuwataka wasimamizi wa barabara kuwachukulia hatua za kisheria mara moja.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Dar es Salaam, Eng. Harun Senkuku amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (njia nane), yenye urefu wa KM 19.2, uliohusisha madaraja ya Kibamba, Kiluvya na Mpiji umekamilika na kinachoendelea sasa ni uboreshaji wa njia ya mwendokasi katika barabara hiyo.

Aidha amezitaja kazi nyingine zinazoendelea kwa sasa kuwa ni ujenzi wa madaraja mawili ya juu eneo la Mbezi Mwisho na Kwa Yusuf kwa ajili ya kupunguza msongamano katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani cha Magufuli, kujenga barabara ya maingilio katika kituo hicho, kujenga kituo cha mabasi ya daladala eneo la Kibamba njia ya Mloganzila na kuongeza taa za kuongozea magari eneo la makutano ya barabara ili kurahisisha uvukaji wa magari na watembea kwa miguu.

Takribani kiasi cha shilingi bilioni 218, zinatarajiwa kutumika katika mradi huo hadi utakapo kamilika baadaye mwezi juni mwaka huu.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment

0 Comments