Ticker

6/recent/ticker-posts

MKUTANO WA NNE WA TUME YA KUDUMU YA PAMOJA KATI YA TANZANIA NA UGANDA WAFUNGULIWA JIJINI KAMPALA, UGANDA

Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Uganda umeanza leo tarehe 17 Januari 2022 katika ngazi ya Wataalamu Jijini Kampala, Uganda.

Mkutano huu wa awali pamoja na mambo mengine utajadili masuala ya ushirikiano yaliyokubaliwa baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda. Mkutano huu utafuatiwa na mkutano katika ngazi ya Makatibu Wakuu utaofanyika tarehe 18 Januari 2022 na utamalizika kwa Mkutano ngazi ya Mawaziri utaofanyika tarehe 19 Januari 2022.

Lengo la Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ni kujadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye mkutano wa tatu uliofanyika mwezi Septemba 2019 jijini Dar es salaam, Tanzania.

Pia, kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika ziara zilizofanywa na Marais wa pande zote mbili katika nyakati tofauti, tangu kumalizika kwa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Uganda.

Vilevile, mkutano huu utashuhudia utiwaji saini wa mikataba takribani sita itakayohusisha sekta mbalimbali za ushirikiano pamoja na kuruhusu maeneo mapya ya ushirikiano. Kadhalika utajadili ushirikiano katika ujenzi wa miradi ya kimkakati unaofanywa na mataifa hayo hususan ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) unaofanywa na Serikali ya Tanzania ambao unatarajiwa kunufaisha nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tanzania na Uganda zinashirikiana katika sekta ya Siasa na Diplomasia, Mawasiliano, Fedha na Uchumi, Nishati, Maendeleo na ujenzi wa Miundombinu, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo na Uvuvi, Maji na Mazingira, Afya na Elimu.

*****************
Waziri wa Nchi, Mambo ya Nje (uhusiano wa Kikanda) wa Uganda akifungua Mkutano wa Nne wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Uganda uliofanyika leo tarehe 17 Januari 2022 katika ngazi ya Wataalamu jijini Kampala, Uganda. Katika Ufunguzi huo Mhe. Mulimba amewahimiza Wataalamu kuwa na namna bora ya kuratibu ufutiliaji wa masuala ya ushirikiano yanayohitaji utekelezaji au utatuzi wa haraka badala ya kusubiri vikao vya waheshimiwa Maraisi.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo ambapo pamoja na mambo mengine Balozi Naimi alieleza kuwa mkutano utajadili na kutathimini utekelezaji katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano, utekelezaji wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaofanywa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na kushuhudia utiwaji saini wa mikataba takribani sita ya ushirikiano baina ya mataifa hayo.
Picha ya pamoja Waziri wa Nchi, Mambo ya Nje (uhusiano wa Kikanda) Mhe. John Mulimba pamoja na viongozi katika ngazi ya Wataalamu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Uganda unaofanyika leo tarehe 17 Januari 2022 jijini Kampala , Uganda.

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Aziz Mlima akifafanua utaratibu wa majadiliano ndani ya mkutano huo.

Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania wakifuatilia mkutano.


Ujumbe kutoka Tanzania.


Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania


Ujumbe kutoka Uganda ukifuatilia mkutano.

Viongozi wakitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ufunguzi wa Mkutano huo.

Post a Comment

0 Comments