Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI JAFO ALEKEZA KILA MWANAFUNZI APANDE MTI, KUUTUNZA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akisikiliza maelezo kuhusu kitalu cha miche kutoka kwa Kaimu Mhifadhi wa Wilaya wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) alipofanya ziara ya kikazi jijini Tanga leo Januari 17, 2022.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akizungumza na watalaamu mbalimbali alipotembelea kitalu cha miche katika Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) alipofanya ziara ya kikazi jijini Tanga leo Januari 17, 2022.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akipanda mti alipotembelea kitalu cha miche katika Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) alipofanya ziara ya kikazi jijini Tanga leo Januari 17, 2022.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Hashim Mgandilwa wakati wa ziara ya kukagua dampo la kisasa la Halmashauri ya Jiji la Tanga leo Januari 17, 2022.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akiwasili katika mradi wa bandari ya kupokelea mafuta eneo la Chongoleani jijini Tanga kwa ajlli ya kukagua uzingatiaji wa Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) leo Januari 17, 2022.

(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

************************

Na Robert Hokororo, Tanga

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo ameelekeza kila mwanafunzi apande mti, kuusimamia na kuutunza hatua itakayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Dkt. Jafo ametoa maelekezo hayo leo Januari 17, 2022 jijini Tanga wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua na kuhamasisha shughuli mbalimbali za hifadhi na utunzaji wa mazingira.

Alisema kuwa upungufu wa miti umekuwa chanzo cha kiwango cha mvua kimepungua na joto limeongezeka kwa kasi hali iliyosababisha ukame ambao matokeo yake baadhi ya wanyama wanakufa.

Kwa mantiki hiyo alisema kuwa kuna umuhimu wa kuwajengea utamaduni wa kupanda miti watoto wa shule ili kuwa na kizazi chenye kujali na kupenda mazingira.

“Pamoja na maelekezo ya Serikali ya Serikali ya kupanda miti milioni moja na nusu kwa kila halmashauri ambayo lengo ni miti milioni 276 kwa halmashauri zote 139 lakini kila mwanafunzi kuanzia chekechekea, msingi, sekondari akipanda mti mmoja na kuusimamia kwa mwaka mzima ndio utakuwa mkombozi wetu kukabiliana na changamoto hizi za kimazingira,” alisema.

Aidha, Waziri Jafo aliwaelekeza viongozi wa mikoa na wilaya kusimamia kikamilifu zoezi la usafi wa mazingira na kusema kuwa ni aibu kwa majiji makubwa kuwa machafu.

Alisisitiza kuwa maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa kitaifa kuhusu usafi wa mazingira yatekelezwe na usafi katika siku za Jumamosi uwe ni utamaduni na uendelee kushika kasi.     

Akitembelea dampo la kisasa la Jiji la Tanga ambapo alionesha kuridhishwa na namna wanavyoshughulikia taka ngumu na kuwapongeza viongozi wanaosimamia dampo hilo.

Hivyo, Waziri huyo aliwataka viongozi wa halmashauri zingine ambazo zimenufaika na miradi ya ujenzi wa madampo ya kisasa kuhakikisha wanayasimamia ipasavyo.

Katika hatua nyingine waziri alifanya ziara katika eneo la Chongoleani ambako kunakotarajiwa kujengwa bandari ya kupokelea mafuta ili kujiridhisha uzingatiaji wa maelekezo ya Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA).

Aliwataka wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na watalaamu kutoka Mamlaka ya Bandari kuhakikisha maelekezo ya EIA yanazingatiwa ili mradi huo uwe endelevu na rafi kwa mazingira.

Post a Comment

0 Comments