Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA SULUHU AZUNGUMZA NA VIONGOZI WA WAMACHINGA WA MKOA WA DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Wamachinga wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam leo tarehe 25 Januari, 2022. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Taifa Bw. Stephen Lusinde mara baada ya kuzungumza na viongozi hao wa Wamachinga Ikulu Jijini Dar es Salaam leo 25 Januari, 2022. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha na Viongozi mbalimbali wa Wamachinga kutoka Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam leo tarehe 25 Januari, 2022.

**************************

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inatambua rasmi Wamachinga kama kundi maalumu na lipo katika Mipango mbalimbali ya maendeleo ya Serikali kwa kundi la vijana.

Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 25 Januari, 2022 wakati akizungumza na viongozi wa Wamachinga wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Samia amesema uwepo wa kundi hilo maalum la Wamachinga limeisaidia Serikali kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na kuinua uchumi wa nchi.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewapongeza Wamachinga kwa kukubali wito wa kuzungumza nao na kuwashukuru kwa kuonesha uungwana na uzalendo wakati wa utekelezaji wa agizo la kuwaondoa katika maeneo ya pembezoni mwa barabara na kukubali kupangwa katika maeneo waliyotengewa.

Vile vile, Mhe. Rais Samia amesema sababu ya kuwaondoa Wamachinga maeneo ya barabarani ni kuepusha msongamano, vitendo vya wizi pamoja kufanya mandhari ya Jiji la Dar es Salaam yawe masafi na ya kuvutia.

Pia, Mhe. Rais Samia amesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko la Kariakoo ambalo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kutumiwa na Wamachinga kati ya 2,500 hadi 4,000, hivyo kutoa nafasi kwa wafanyabiashara hao waliokosa maeneo kupata maeneo ya kufanyia biashara.

Mhe. Rais Samia ameridhia ombi la Wamachinga la kutaka kushirikishwa katika ujenzi wa masoko na hivyo kumuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla kuwashirikisha katika ujenzi wa soko jipya utakaoanza katika eneo la Jangwani.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuandaa mpango maalumu wa kuwawezesha Wamachinga kunufaika na mikopo ya asilimia 10 pamoja na kuzitumia fedha za Halmashauri kufanya maboresho katika maeneo ambayo Wamachinga wanaendesha biashara zao.

Kwa upande mwingine, Mhe. Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) kuhakikisha inaratibu uwepo wa daladala ambazo zitawezesha wananchi kufika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Wamachinga.

Mhe. Rais Samia amewajulisha Wamachinga kuwa baada ya kukamilika kwa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na kukamilika kwa ujenzi wa masoko, Serikali itaandaa mfumo wa vitambulisho vya wamachinga ambavyo vitakuwa na taarifa muhimu zitakazowawezesha kupata mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri na taasisi za kifedha.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka wamachinga kujiandaa kulipa kodi zitakazowiana na biashara zao pindi watakapoanza kutumia masoko mapya ili fedha hizo ziweze kutumika kuboresha huduma za wamachinga.

Halikadhalika, Mhe. Rais Samia amewataka Wamachinga kuacha kutumiwa na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa hasa wa Kariakoo kwa kuwa kitendo hicho kinaikosesha mapato Serikali.


Kuhusu majanga ya moto katika Masoko, Mhe. Rais Samia amewataka Wamachinga kujisimamia na kuepukana na masuala yanayohatarisha usalama wa masoko na kuhakikisha ujenzi wa vibanda vipya vya soko la Karume unazingatia uwepo wa nafasi zitakazowezesha magari ya zimamoto kupita wakati majanga yanapotokea

Post a Comment

0 Comments