Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUFUNGUA BARABARA YA CHANKERE-KAGUNGA, KIGOMA


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) akipewa maelezo na Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoani Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, kuhusu ujenzi barabara ya Chankere - Kagunga yenye urefu wa Kilomita 45 itakayojengwa kwa kiwango cha zege, mkoani Kigoma.


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (mwenye skafu) na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, wakikagua barabara ya Chankere – Kagunga, itakayojengwa kwa kiwango cha zege, mkoani Kigoma.


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) akieleza nia ya Serikali ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa na barabara ya Chankere – Kagunga, yenye urefu wa kilomita 45 kutokana na umuhimu wake kiuchumi, wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Kigoma. Kulia ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa na kushoto ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mhe. Assa Makanika.


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia) na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakizungumza jambo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua barabara ya Chankere – Kagunga, itakayojengwa kwa kiwango cha zege, mkoani Kigoma.


Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mhe. Assa Makanika (kushoto), akieleza umuhimu wa barabara ya Chankere – Kagunga, yenye urefu wa kilomita 45 hasa katika masuala kuwasaidia wananchi kufika kwa urahisi kupata huduma za afya. Wa pili kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).


Muonekano wa barabara ya ya Chankere – Kagunga iliyopo Wilaya ya Kigoma, yenye urefu wa kilomita 45, ikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Kigoma)

******************************

Na. Saidina Msangi na Peter Haule, WFM, Kigoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameahidi kuwa Serikali itatafuta fedha za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Chankere – Kagunga mkoani Kigoma yenye urefu wa Kilomita 45 itakayojengwa kwa kiwango cha zege.

Ahadi hiyo ameitoa Mkoani Kigoma wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo ina tija kwa Taifa ikizingatiwa kuwa itatumiwa na wananchi na watalii wanaokwenda kutembelea hifadhi ya Gombe ambayo ni muhimu katika kukuza uchumi na pato la Taifa.

“Mhe. Rais anasisitiza tukafungue maeneo ambayo hayajafunguliwa tangu uhuru, hiyo imekuwa kiu yake ndio maana fedha nyingi zimeelekezwa kwa Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) na kuwezesha kufungua barabara nyingi ndani ya miezi sita ambazo hazikuwahi kuguswa”, alieleza Dkt. Nchemba

Alisema kuwa Serikali itaweka uzito kuhakikisha barabara hiyo inakamilika ili kufungua maeneo hayo na kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itashirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuweka mipango ya kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo.

Dkt. Nchemba alisema kuwa, kutembelea barabara hiyo kumemuwezesha kupata picha halisi ya barabara hiyo hivyo itasaidia katika kufanya maamuzi kwa kutoa kipaumbele katika utekelezaji wake.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema kuwa barabara hiyo ina changamoto kubwa ya kijiografia lakini ni muhimu kwa uchumi wa Taifa hivyo Wizara imeweka mikakati kuwezesha ujenzi wa barabara hiyo.

“Barabara ina changamoto kubwa lakini ni muhimu kwa ukuaji uchumi, hivyo nia ya Serikali ni kuweka mikakati ya kujenga barabara hiyo licha ya changamoto zilizopo”, alieleza Prof. Mbarawa.

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mhe. Assa Makanika, amewashukuru Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kwa kufika kuona barabara hiyo muhimu kwa kuwa inatumiwa na watu wengi wanajishughulisha na shughuli za kiuchumi zikiwemo za uvuvi.

Alisema kwa sasa wananchi wanatumia zaidi ya saa saba kusafiri kwa njia ya maji kwenda Kigoma mjini, kutokana na kadhia hiyo baadhi ya wagonjwa hupoteza maisha kabla ya kufikishwa hospitalini kupata huduma za afya.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa barabara (Tanroad) mkoa wa Kigoma Mhandisi, Narcis Choma, alisema kuwa barabara hiyo ikimalizika itasaidia kufungua mawasilian na nchi ya Burundi na kwa sasa zinahitajika takribani shilingi bilioni 30 ili barabara hiyo iweze kuanza kutumika.

Post a Comment

0 Comments