Ticker

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI SEKTA YA AFYA NCHINI WATAKIWA KUWA WAZALENDO NA KUFANYA KAZI KWA WELEDI

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Meja Jenerali Gabriel Mhidze Dkt (kushoto) akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa mafunzo maalumu ya kusafisha damu (dialysis), yaliyotolewa kwa madaktari na wauguzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala, ili kuwajengea uwezo na umahiri katika kutumia mashine mpya na za kisasa zilizonunuliwa na MSD na zinatarajiwa kusambazwa katika hospitali mbalimbali nchini. Hafla ya kukabidhi vyeti kwa wahitimu ilifanyika Hospitali ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam jana.
Maofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakiwa kwenye hafla hiyo.
Wahitimu wakionesha vyeti vyao baada ya kukabidhiwa.
Picha ya pamoja na wahitimu.


****************

Na Mwandishi Wetu.



MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Meja Jenerali Gabriel Mhidze (Dkt) amewataka Watumishi wa kada ya afya nchini kuwa Wazalendo na kufanya kazi zao kwa weledi, ili kwa Pamoja kuweza kutimiza adhima ya serikali ya kuboresha afya za wananchi, kupitia miradi mbalimbali ya afya inayoanzishwa nchini.

Meja Jenerali Gabriel Mhidze (Dkt) amesema iwapo kada hiyo ya afya itakubali mabadiliko chanya yanayofanywa na serikali, kutakuwa na ahueni kubwa kwa wananchi, kwani serikali kupitia wizara ya afya imedhamiria kupunguza gharama za matibabu, kuboresha miundombinu ya afya, sambamba na kusogeza huduma mbalimbali za afya karibu na wananchi, ikiwemo huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa figo nchini.

Afande Mhidze ametoa rai hiyo hii leo tarehe 6/01/2022 kwenye Hospitali ya jeshi ya Lugalo, wakati akifunga mafunzo maalum ya Kusafisha damu (dialysis), yaliyotolewa kwa watumishi yaani madaktari, wauuguzi na mhandisi vifaa tiba; kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala, ili kuwajengea uwezo na umahiri katika kutumia mashine mpya na za kisasa zilizonunuliwa na MSD na zinatarajiwa kusambazwa katika hospitali.

Pamoja na rai hiyo, Afande Mhidze amewatunuku vyeti wahitimu hao na kuwataka kuwa mabalozi wazuri huko waendako, kwa kueneza mazuri waliyojifunza, ili hospitali zingine ziweze kuhamasika na kuanzisha huduma hizo za kibingwa katika maeneno yao.

Dkt. Linda Ezekiel, Mratibu wa Huduma za magonjwa ya Figo nchini amemshukuru Meja Jenerali Gabriel Mhidze (Dkt), na wadau mbalimbali kwa utayari wao katika kuleta mapinduzi katika matibabu ya kusafisha damu nchini huku akiushukuru uongozi wa Hospitali ya Jeshi Lugalo chini ya Brigedia Jenerali. Dkt.Fredy Kivamba kwa kukubali kuwa mwenyeji mafunzo hayo.

Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi, ameelezea uwepo kwa ongezeko kubwa la wagonjwa wenye matatizo ya figo nchini, huku akiwataka wataalamu kufanya kazi zao kwa nidhamu na weledi ili lengo lililokusudiwa na serikali kupitia mafunzo hayo liweze kutimizwa. Sambamba na hilo amewataka wananchi kubadili mitindo hatarishi ya Maisha, ikiwa ni Pamoja na kupima afya zao mara kwa mara ili kujua yanayowasibu mapema pamoja na kufanya mazoezi.

Mwakilishi wa wahitimu hao, Dkt.Pantaleo Joseph ameishukuru serikali kwa kuandaa mafunzo hayo adhimu, na kuupongeza uongozi wa Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo huku wakiomba mafunzo hayo yawe endelevu na yawafikie wenzao walioko katia vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya, kwani yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma na kuokoa Maisha ya wananchi.

Post a Comment

0 Comments